Siasa

Munya adai alijaribu kumwokoa Kindiki akafeli

May 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

DAVID MUCHUI na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Kilimo Peter Munya ameelezea jinsi alivyojaribu kumnusuru Seneta wa Tharaka-Nithi Kithure Kindiki asing’olewe kutoka wadhifa wa Naibu Spika lakini akafeli.

Alisema hii ni baada ya kupewa ushahidi kwamba Profesa Kindiki, na wengine ambao walivuliwa nyadhifa zao na Jubilee walihujumu ajenda ya serikali katika seneti.

“Kwa hivyo, singeweza kuokoa ndugu yangu Profesa Kindiki kwa sababu ilikuwa ni wazi alikuwa miongoni mwa wale ambao huhujumu serikali ambayo wanapaswa kutetea katika bunge hilo,” Bw Munya akasema.

Waziri huyo wa Kilimo alisema alipata ushahidi kuwa Profesa Kindiki, na wenzake Kipchumba Murkomen na Susan Kihika, walipinga hatua ya Serikali kutwaa majukumu manne ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Bw Munya alisema hatua hiyo ilikuwa kinyume na matamanio ya Rais Uhuru Kenyatta ambaye pia ndiye kiongozi wa Jubilee.

Alisema hayo alipokutana na viongozi wa vyama vya ushirika vya wakulima wa kahawa katika Kiwanda cha Kahawa cha Meru New KPCU Jumamosi.

Hata hivyo, waziri Munya alipongeza wimbi linaloendelea katika chama cha Jubilee dhidi ya wabunge na maseneta waasi ambao alisema wanahujumu ajenda ya maendeleo ya Rais Kenyatta.

“Rais Kenyatta amejitolea kurejesha sura ya Nairobi kama zamani, ikizingatiwa kuwa ndilo jiji kuu la Kenya na yeyote anayepinga au kuhujumu ajenda hii ni adui sio tu wa serikali bali taifa la Kenya kwa ujumla,” Bw Munya akakariri.

Bw Munya pia alimshutumu Naibu Rais William Ruto kwa kutumia baadhi ya wabunge wandani wake kumpiga vita bosi wake, Rais Kenyatta.

“Huwezi kumkosea heshima mkubwa wako ukidai hiyo ni demokrasia. Hata katika mataifa yaliyoendelea kidemokrasia kama Amerika, huwezi kumwona Makamu wa Rais Mike Pence akiwachochea wabunge kumpiga vita Rais Trump. Hii sio demokrasia. Ikiwa wadogo wako wanakupiga vita, huwezi kuketi na kutizama,” waziri huyo wa kilimo akaeleza.

Bw Munya aliwashutumu baadhi ya wabunge kutoka kaunti za Meru, Tharaka-Nithi na Embu ambao alisema wamegeuza suala la kutimuliwa kwa Seneta Kindiki kuwa “siasa za kiukoo.”

“Juzi niliona baadhi ya watu wakidai kuwa eneo la Mlima Kenya Mashariki sasa limetengwa. Mabadiliko yanayotekelezwa hayafai kudunishwa kwa kuchukuliwa kama siasa za kiukoo. Serikali inapania kuondoa viunzi vinavyoizuia kutoa huduma kwa Wakenya,” akasema.

Takrina wabunge 10 wakiongozwa na Seneta wa Meru Mithika Linturi walimtetea Seneta Kindiki na kumshutumu Rais Kenyatta kwa kile walisema ni kusaliti wapigakura wa eneo hilo.