Siasa

'Murunga alihudumia wakazi wa Matungu kwa moyo wa kujitolea'

November 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

VIONGOZI kadha wa kisiasa nchini wametuma risala za rambirambi kwa familia, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Mbunge wa Matungu Justus Murunga.

Wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanasiasa hao walimtaja mwendazake kama kiongozi mchapa kazi, mwenye maoni na aliyehudumia taifa hili na watu wa Matungu kwa moyo wa kujitolea.

“Mheshimiwa Murunga pia alikuwa kiongozi aliyetilia maanani miradi yenye kuwapa uwezo watu wake. Ama kwa hakika watu wa Matungu watamkosa. Sisi kama Wakenya pia tutakosa upendo na mchango wake katika juhudi za kuwaleta pamoja watu wa eneo la Magharibu,” akaeleza Dkt Ruto kupitia Twitter.

Kwa upande wake Bw Odinga alisema: “Nasema pole kwa watu wa Matungu kwa kumpoteza kiongozi wao shapavu wakati ambapo walihitaji huduma zake zaidi; katika muhula wake wa kwanza. Rambirambi zangu ziwefikia familia, jamaa na marafiki wa Mheshimiwa Justus Murunga. Mungu apumzishe roho ya pema daima.”

Gavana wa Kakamega naye alimtaja mwendazake kama kiongozi shupavu aliyeshirikiana naye kutekeleza miradi ya mengi ya maendeleo katika eneo la Matungu.

“Nimehuzunishwa zaidi na kifo chake ambacho kimepokonya kaunti ya Kakamega kiongozi mwenye maoni ambaye atakoswa zaidi kutokana na michango yake katika maendeleo.” akasema Bw Oparanya.

Wengine walituma risala zao ni Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, Mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali, Christopher Aseka (Khwisero), aliyekuwa senata wa Kakamega Bonny Khalwale miongoni mwa wengine.

Bw Murunga alifariki Jumamosi jioni alipokuwa akikimbizwa kupelekwa Hospitali ya St Mary’s, Mumia baada ya kukumbwa na matatizo ya kupumua.

Mbunge huyo alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, Kisumu kwa majuma mawili yaliyopita akiugua ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.

Aliondoka hospitalini mnamo Alhamisi na amekuwa akitunzwa nyumbani kwake katika kijiji cha Emakunda, eneobunge la Matungu, Kaunti ya Kakamega hadi Jumamosi alipoanza kupatwa na matatizo ya kupumua.

Marehemu Murunga alizaliwa mnamo mnamo 1961. Amekuwa akiwania kiti cha ubunge cha Matungu tangu 2002 lakini hatimaye akashinda mnamo 2017 kwa tiketi ya chama cha Amani National Congress (ANC) baada ya kumbwaga David Were. Bw Were alihudumu kati ya 2007 na 2013.

Katika bunge la sasa Bw Murunga amekuwa akihudumu kama mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo na Ufugaji.