Siasa

Mwaniaji ubunge Kibra kwa tiketi ya ODM kuamuliwa hadharani

August 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MGOMBEAJI wa kiti cha ubunge wa Kibra kwa tiketi ya chama cha ODM atajulikana kesho Jumapili wakati wa mkutano wa hadhara utakaoongozwa na kiongozi wa chama hicho Raila Odinga katika uwanja wa Kamukunji eneobunge hilo.

Chama hicho kilisema Ijumaa kwamba Bw Odinga atatumia jukwaa hilo kuwapa wagombeaji wote nafasi ya kuuza sera zao kwa wakazi wa eneobunge hilo kuamua “aliye bora kati yao”.

“Katika mkutano huo kiongozi wa chama atawajulisha kwa wakazi wale wote waliomba kuwania kiti hicho tiketi ya ODM kuchukua nafasi ya marehemu Ken Okoth kama mbunge. Wafuasi wote wa ODM na wapigakura wamealikwa katika mkutano huo Jumapili Agosti 25, 2019,” ikasema taarifa iliyotumwa kwa vyumba vya habari na msemaji wa Bw Odinga Dennis Onyango.

Mkutano huo utafanyika katika uwanja wa Kamukunji katika eneobunge hilo.

Tangazo hilo lilitolewa baada ya Bw Odinga kuongoza mkutano wa Kamati Kuu ya Usimamizi (CMC) ya chama hicho ulioitishwa kujadili mfumo ambao utatumia kuteua mgombeaji wa ODM.

Wakazi wapewa usemi na uhuru

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba mkutano huo uliamua kuwapa wakazi wa Kibra usemi na uhuru katika kaumua yule wanayemtaka “bila kuingiliwa na uongozi wa chama.”

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) tayari imetangaza kuwa uchaguzi huo utafanyika Novemba 7, 2019, na vyama vinavyonuia kudhamini wagombeaji vimepewa makataa ya hadi Septemba 10 kukamilisha uteuzi wa wagombeaji wao.

Duru zinasema kuwa jumla ya watu tisa wanataka kuwania kiti hicho kwa tiketi ya ODM, chama kilicho na wafuasi wengi zaidi eneo hilo.

Wao ni kakake marehemu Ken Okoth ambaye ni Imran Okoth (pichani), aliyekuwa Mbunge wa Embakasi Kusini Irshad Sumra, kiongozi wa vijana wa ODM eneo la Kibra Benson Musungu, Katibu Mpanga Ratiba wa ODM eneobunge la Kibra Sigar Agumba na aliyekuwa diwani wa wadi ya Sarang’ombe Owino Kotieno.