Siasa

Mzozo watokota ngazi ya juu uongozi wa Ford-Kenya

June 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na RICHARD MUNGUTI

MZOZO wa uongozi wa chama cha Ford-Kenya umetokota Jumatano baada ya jopo la kuamua mizozo ya vyama vya kisiasa (PPDT) kukataa kuzima utambuzi wa Mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi kuwa kiongozi mpya wa chama hicho.

Badala ya kumzuia Msajili wa Vyama vya kisiasa katika afisi ya Mwanasheria Mkuu Bi Anne Nderitu kusajili kundi la Wamunyinyi kuwa viongozi wa Ford-Kenya, wanachama wa PPDT waliamuru kesi iliyowasilishwa mbele yao isikizwe Ijumaa, Juni 12, 2020.

Chama cha Ford-Kenya kupitia mawakili Eunice Lumallas, Nelson Havi, Ben Millimo na Dkt John Khaminwa kiliomba PPDT kisitishe hatua ya kuandikishwa kwa wanachama wanaongozwa na Bw Wamunyinyi kuwa maafisa wapya wa ngazi ya juu Ford-Kenya.

Jopo hilo linaloongozwa na Desina Mugo, Milly Lwanga na Adelaide Mbithi liliratibisha kuwa ya dharura kesi iliyowasilishwa na Ford-Kenya.

Akiwasilisha ushahidi mbele ya jopo hilo Bw Havi alisema kuwa mnamo Mei 31, 2020, katika hoteli ya Radisson Blue jijini Nairobi mapinduzi ya uongozi wa chama cha Ford-Kenya yalifanywa na kumng’atua uongozini Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

“Baada ya kumtimua uongozini Bw Wetang’ula kundi la Wamunyinyi liliwasilisha majina ya uongozi mpya wa Ford-K kwa msajili wa vyama kuandikishwa mnamo Juni 2, 2020,” Bw Havi ameeleza jopo hilo.

Alisema msajili wa vyama alikataa kutambua majina ya Bw Wamunyinyi na wenzake kisha akaamuru kundi hilo pamoja na lile linaloongozwa na Bw Wetang’ula wafuate Katiba cha chama cha Ford-Kenya.

Jopo hilo lilielezwa siku hiyo hiyo ya Juni 2 maafisa wa kuu wa Ford-K walikutana na kujadili suala la utovu wa nidhamu wa Wamunyinyi na wenzake na wakatimuliwa uongozini wa chama hicho.

Jopo lilielezwa kuwa baada ya kuondolewa uongozini, majina ya kundi hilo la Wamunyinyi yalipelekwa kwa msajili wa vyama yaondolewe katika sajili ndipo ikaguduliwa kulikuwa na barua iliyoandikwa kumwondoka Wetang’ula kuwa kinara wa Ford-K.

Akiomba jopo hilo lisitishe kusajiliwa kwa kundi la Wamunyinyi hadi kesi hiyo isikizwe na kuamuliwa, Bw Havi aliyepia Rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK), alisema katiba itakiukwa endapo msajili atabadilisha uongozi wa Ford-Kenya.

Wakili huyo alisem kuna utaratibu uliowekwa wa kufanya uchaguzi wa Ford-K na “ haukufuatwa ila mageuzi yalitekelezwa na kundi ndogo la viongozi wa chama hicho.”

Wakili huyo aliomba jopo liamuru msajili wa vyama awache majina ya zamani ya uongozi wa Ford-Kenya yasalie jinsi yalivyo Bw Wetang’ula akiwa kinara.

Pia aliomba mzozo huo wa uongozi upelekwe kuamuliwa na kamati ya chama hicho cha Ford-Kenya.

Katika mageuzi yaliyofanywa chamani hicho Mbunge wa Tongareni Dkt David Eseli Simiyu aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Bw Wamunyinyi aliye pia Mbunge wa Kanduyi akatawazwa kuwa Mwenyekiti Mpya wa Ford-Kenya.

Dkt Khaminwa aliambia jopo hilo kwamba Ford-Kenya iliwasilisha kesi mahakamani Juni 4 kupinga kutambuliwa kwa kundi la Wamunyinyi lakini ikaorodheshwa kusikizwa Juni 16.

“ Naomba hii jopo isitishe kutambuliwa kwa kundi la Wamunyinyi. Iwapo hakuna maagizo yatatolewa kumzuia Bi Nderitu kusajili kundi hili la mapinduzi basi katiba ya 2010 kuhusu vyama vya kisiasa na ile ya Ford-Kenya zitakuwa zimekandamizwa,” alirai Dkt Khaminwa anayemwakilisha Wetang’ula akiwa na Bw Havi.

Mawakili hao walisema kuwa wako na uhakika hati zilizotumika kusajili kundi la Wamunyinyi sio halali.

Kupitia chapisho kwenye gazeti rasmi la serikali, msajili wa vyama vya kisiasa, Bi Anne Nderitu alitoa notisi ya kuidhinisha kuteuliwa kwa Wamunyinyi kama kiongozi mpya wa chama hicho.

Aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Ford-Kenya Chris Mandu Mandu alitemwa na wadhifa huo kupokezwa Bi Josephine Maungu.

“Yeyote ambaye ana malalamishi kuhusu mabadiliko yanayokusudiwa na chama hiki, anahitajika kuandikia afisi ya msajili wa vyama kwa muda wa siku saba baada ya notisi hii,” akasema Bi Nderitu.

Matukio haya yanamzidishia Bw Wetang’ula masaibu, ikikumbukwa aling’olewa kutoka wadhifa wa Kiongozi wa Wengi katika Seneti mwaka wa 2018.

Hii ni licha ya kuwa alishikilia wadhifa huo kwa msingi wa kuwa mmoja wa vigogo wa muungano wa Nasa.

Katibu Mkuu Dkt Eseli Simiyu ambaye pia ni mbunge wa Tongaren na Bw Wamunyinyi pamoja na wanachama wengine wa NEC walibadilisha uongozi chamani.

Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati alikuwa miongoni mwa viongozi ambao walihudhuria kikao hicho na kumshutumu Bw Wetang’ula kwa kuongoza chama kiimla, kutoshinikiza umoja chamani na pia kukosa kukivumisha na kukipa sura ya kitaifa.