Nitaiga Magufuli kuzima ufisadi, asema Maraga
JAJI Mkuu Mstaafu David Maraga ametangaza kampeni kali ya kupambana na ufisadi endapo atachaguliwa kuwa Rais, akiahidi kuhakikisha maafisa wa umma wanawajibika moja kwa moja kwa wananchi kwa kila shilingi inayowekwa mikononi mwao.
Akizungumza katika Kaunti ya Tana River wakati wa mkutano wa hadhara na wakazi, Jaji Mkuu mstaafu alieleza kwamba ufisadi umeathiri ukuaji wa taifa, kueneza umasikini, na kudhoofisha imani ya raia na wawekezaji katika taasisi za serikali.
Maraga aliwataka Wakenya kumwamini kwa masuala ya fedha za nchi, akiahidi kugeuza Kenya kuwa uchumi wa kiwango cha kwanza katika muhula wake wa kwanza madarakani.
Alisema uongozi wake utajengwa kwenye uwazi, uwajibikaji, na ushirikishaji wa wananchi katika utawala.
“Mkinichagua mimi, nataka mjue kwamba pesa zenu zitakuwa salama. Ikiwa shilingi moja itaibiwa kwa niaba yenu, mtu atakayehusika atajibu hadharani. Nitawafanya waelezeWakenya, uso kwa uso, kwa nini walishindwa kutimiza majukumu yao,” alisema, akishangiliwa na umati wa watu.
Bw Maraga alisema hatakubali ufisadi katika utawala wake, akisisitiza kuwa Waziri yeyote au afisa wa serikali akihusishwa na ufisadi atafukuzwa mara moja na kufikishwa mahakamani.
“Serikali yangu haitavumilia ufisadi. Ikiwa waziri wangu yeyote au maafisa watapatikana wakiiba pesa za umma, sitawalinda. Watafikishwa mbele ya sheria na wananchi,” alisema.
Maraga alilinganisha mtindo wake wa uongozi na ule wa hayati Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli, ambaye utawala wake ulijulikana kwa unyenyekevu, nidhamu, na vita vikali dhidi ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilmali za umma.
Alisema Wakenya wamezoea “maneno makali na kelele kubwa” kutoka kwa wanasiasa bila matokeo halisi, akisisitiza kwamba sasa taifa linahitaji kiongozi wa vitendo, si maneno.
“Tumezungumza sana katika nchi hii. Viongozi hupiga kelele, wanaahidi kuzima ufisadi, kisha wanatulia baada ya kupata madaraka. Wakenya wamezoea kutafsiri kelele kama nguvu za kisiasa. Nataka kuwathibitishia kuwa uongozi sio kuhusu kelele bali ni kuhusu kuchukua hatua,” alisema.
Maraga alikanusha madai kwamba yeye ni mpole sana kwa siasa kali, akionya kuwa wale wanaochukulia utulivu wake kama udhaifu watashangaa mara atakapokuwa madarakani.
“Watu wengine hufikiria mimi ni mpole kwa sababu ninazungumza kwa utulivu. Lakini kumbuka, si mnyonge aliyefuta uchaguzi wa urais mwaka 2017. Uamuzi huo ulikuwa mmoja wa hatari na mgumu zaidi katika historia ya Kenya. Niliuchukua kwa sababu ilikuwa jambo sahihi,” alisema.
Mnamo 2017, Mahakama ya Juu chini ya Maraga ilitoa uamuzi wa kihistoria kufuta uchaguzi wa urais, ikibainisha dosari na ukiukaji wa sheria katika mchakato wa uchaguzi.
Maraga pia alikumbuka uamuzi wake wa kupendekeza kuvunjwa kwa Bunge mwaka 2020 kwa kushindwa kutimiza kanuni ya usawa wa jinsia, akisema kilikuwa kitendo kingine cha ujasiri.
Alisema matukio hayo mawili katika kazi yake ya kisheria ni ushahidi kwamba si mtu rahisi kutishwa na shinikizo za kisiasa, akisisitiza kwamba urais wake utajengwa juu ya msingi ule ule wa uadilifu, ujasiri, na uhuru.
Maraga aliongeza kuwa ufisadi ni kizuizi kikuu cha maendeleo ya Kenya, ukigharimu taifa mabilioni ya pesa kila mwaka.
Aliahidi kuvunja mitandao ya ufisadi ambayo imekua kwa miongo ndani ya mashirika ya serikali.
“Hatuwezi kuwa uchumi wa kiwango cha kwanza ikiwa ufisadi utaendelea kufyonza rasilmali zetu. Utawala wangu utaweka kipaumbele mifumo inayozuia wizi kabla haujatokea, sio tu kuchukua hatua baada ya matukio,” alisema.