Njama ya Ruto kurarua roho ya Mlima
ENEO la Mlima Kenya, ambalo lilikuwa ngome ya kisiasa iliyoungana na kutoa mwelekeo thabiti wa kura katika uchaguzi wa urais, sasa linakabiliwa na mgawanyiko mkubwa ambao haujawahi kushuhudiwa, kwa hisani ya ujanja wa kisiasa wa Rais William Ruto.
Kuibuka kwa vyama vingi vya kisiasa vilivyo na mizizi katika eneo hili, ikiwa ni pamoja na chama kipya cha Democracy for the Citizens Party (DCP) cha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Jubilee cha Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, People’s Liberation Party (PLP) cha Martha Karua, The Service Party (TSP) cha Mwangi Kiunjuri, Chama Cha Kazi (CCK) cha Moses Kuria, na Party of National Unity (PNU) cha Peter Munya, kunaashiria ubabe mkali wa kuwania ushawishi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Ripoti zinaonyesha kuwa zaidi ya vyama 30 vya kisiasa, vingine vikiwa vilisajiliwa hivi majuzi, vina makao katika eneo hili lililo na wapiga kura wengi, vikilenga uchaguzi wa 2027, huku washauri wa Rais William Ruto wakilenga kufadhili wagombeaji urais kutoka mlima Kenya.
Mbali na DCP, Jubilee, PLP, TSP, CCK na PNU, vyama vingine katika eneo hilo ni pamoja na: Usawa Kwa Wote Party ya aliyekuwa Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria, Tujibebe Wakenya inayohusishwa na Waziri wa ICT William Kabogo, Ubuntu People’s Forum inayohusishwa na Waziri wa Biashara Lee Kinyanjui, Democratic Party, Farmers Party, Safina Party ya Jimi Wanjigi, Kenya National Congress, The New Democrats Party, The National Party (TNP), The National Alliance, Mwangaza Party, na National Democratic Movement (NDM).
Wachambuzi wa siasa wanasema mgawanyiko huu huenda pia unasababishwa na kutamauka kisiasa, mabadiliko ya kizazi, na mwelekeo mpya wa kiitikadi.
Ingawa United Democratic Alliance (UDA) cha Rais Ruto bado kina ushawishi mkubwa katika eneo hili, mzozo kati yake na naibu wake wa zamani, Bw Gachagua, umeongeza hisia za usaliti na kutengwa hasa miongoni mwa viongozi wa Mlima Kenya wanaohisi kutengwa licha ya kumuunga mkono mwaka 2022.
Chama cha DCP cha Bw Gachagua kinawasilishwa kama chombo kipya cha kurejesha utambulisho wa kisiasa wa eneo hilo.
“Tumemalizana na UDA. Kamwe hatutakwenda kwenye uchaguzi bila chama chetu. Mara ya mwisho, tulienda harusi kwa gari la bw harusi, lakini tulipofika mtoni akatuambia tushuke na akawapandisha wengine,” alisema.
Hata hivyo, kukumbatiwa kwa chama kunakabiliwa na upinzani kutoka PLP, Jubilee, na PNU.
Kila chama kinajiimarisha mashinani katika kaunti muhimu kama Nyeri, Murang’a, Kiambu, Kirinyaga, Nyandarua, Meru, Embu, Tharaka Nithi, Nakuru, na Laikipia.
Chama cha Jubilee cha Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, bado kina umaarufu eneo hili. Uongozi wake unasema bado hakijafa na kinatumai hisia za kupinga Ruto na kumbukumbu za enzi zake zitasaidia kukiimarisha.
Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni ameahidi kuwa chama hicho kitaunga mkono aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i, huku akijitenga na kambi ya Bw Gachagua.
Kuongezeka kwa vyama vya kisiasa katika eneo hilo kumeibua hofu ya kudhoofisha uwezo wa Mlima Kenya kujadili kwa nguvu katika siasa za kitaifa.
Wachambuzi wa kisiasa wanaamini kuwa “Mlima Kenya uliogawanyika hauwezi kujadili kwa maana katika meza ya kitaifa.”
Eneo hilo, ambalo limetoa marais watatu na mara nyingi limekuwa likipiga kura kama kundi moja, sasa iko hatarini kuingia 2027 likiwa kama nyumba iliyogawanyika, licha ya kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura.
Wakati wanasiasa wakuu wakijaribu kurithi Mlima, mustakabali wa umoja wa eneo hilo bado haujulikani.Mchambuzi wa kisiasa Martin Oloo anasema kuwa siasa za Kenya zimepata mwelekeo mpya kufuatia makubaliano ya kisiasa kati ya UDA ya Rais Ruto na ODM ya Raila Odinga.
Anasema usaliti wa ghafla na kujiondoa kwa ODM kutoka muungano wa Azimio unaonyesha haja ya kuunda muungano wa kisiasa wa muda mrefu zaidi ya 2027.
“Ili Ruto na Raila washindwe mwaka 2027, lazima kuwe na muungano mkubwa wa kisiasa mbadala kama ule wa NARC dhidi ya KANU mwaka 2002. Ikiwa upinzani hautajiunga na kuweka mgombea mmoja, Ruto na Raila watafadhili wagombeaji wa urais wachache watakaopunguza kura,” anasema Bw Oloo.
Anaongeza kuwa kwa sasa, Bw Gachagua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na viongozi wengine wa upinzani “hawana chaguo ila kuungana.”
“Lazima wajitolee kwa ajili ya kila mmoja. Lazima wafanye hesabu na kuwa na mgombeaji mmoja, si kwa sababu ndiye bora zaidi, bali kwa sababu anaweza kuwa msingi wa kumshinda Ruto”
Baadhi ya watu binafsi, ambao huenda hawana nia ya kugombea nyadhifa za kisiasa, pia wameingia katika mtindo wa hivi karibuni wa kusajili vyama vipya kwa nia ya kuviuza kuelekea uchaguzi wa 2027.
Uuzaji na ununuzi wa vyama vya kisiasa umekuwa biashara yenye faida kubwa, hasa kutokana na hofu ya baadhi ya wanasiasa kuhujumiwa kwenye mchujo wa vyama.
Baadhi ya viongozi wakuu wa kisiasa walijikuta bila vyama baada ya makundi pinzani kuondoka na vyeti vya chama.
Matukio haya yamewalazimu wanasiasa wenye tamaa kuwa na vyama vyao ili kujihakikishia tiketi za uchaguzi na pia kwa madhumuni ya mazungumzo ya miungano.