Siasa

Raila akanganya kuhusu BBI

November 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANDISHI WETU

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga, Jumatano alionekana kuchanganyikiwa kuhusu yaliyomo kwenye mswada wa marekebisho ya katiba kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Katika hotuba yake wakati wa kuzindua ukusanyaji sahihi za wapigakura wanaounga mkono mswada huo, Bw Odinga alinena mambo yanayotofautiana na yale yaliyomo kwenye mswada uliowasilishwa kwa Wakenya.

Katika suala la nafasi ya Waziri Mkuu, Bw Odinga alisema hakuna vile nafasi hiyo itamwongeza Rais mamlaka. Kulingana naye, Rais hatakuwa na nguvu za kumsimamisha kazi Waziri Mkuu bali jukumu hilo litakuwa mikononi mwa wabunge.

“Someni kwa umakinifu mtuambie ni wapi tunaleta rais mwenye mamlaka makuu. Ukiwa na waziri mkuu anayeteuliwa na rais lakini anaidhinishwa na bunge, na anaweza tu kuondolewa na bunge, rais ataongezwaje mamlaka? Hiyo inapunguza mamlaka ya rais,” akaeleza.

Lakini, mswada wa BBI unaeleza kuwa mojawapo ya njia ambazo nafasi ya waziri mkuu itabaki wazi ni kama rais ataamua kumtimua.

Kuhusu uhuru wa mahakama, Bw Odinga alisisitiza kuwa mpokeaji malalamishi kuhusu majaji hatakuwa mwajiriwa wa Rais.

Kulingana na maelezo yake, uhuru wa mahakama utaendelea kudumishwa hata afisi ya kupokea malalamishi ya wananchi kuhusu majaji ikibuniwa kwa sababu kutakuwa na jopo la kuhoji wanaotaka kusimamia wadhifa huo, kisha majina matatu yatawasilishwa kwa Rais ambaye atapeleka jina moja bungeni ili aliyemteua ahojiwe kabla ya kuidhinishwa.

Hata hivyo, sehemu ya mswada wa marekebisho ya katiba inayozungumzia suala hilo inasema: “Kutabuniwa afisi ya mpokeaji malalamishi kuhusu mahakama. Rais, akiidhinishwa na Seneti, atamwajiri mpokeaji malalamishi kuhusu mahakama.”

Bw Odinga alitetea afisi hiyo akisema wananchi wanahitaji mahali ambapo wanaweza kupeleka malalamishi yao endapo majajai wanapotoka kimaadili.