Siasa

Raila akubaliana na Ruto kuna pepo wa kupinga serikali Kenya

Na JOSEPH OPENDA December 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga, mnamo Ijumaa Desemba 20 aliunga Rais William Ruto huku akilaumu wakosoaji wa utawala wa Kenya Kwanza kwa kukataa kuona chochote kizuri serikalini.

Japo alikiri kwamba nyakati ngumu za kiuchumi zimeshuhudia kupungua kwa imani ya umma kwa taasisi za serikali na kuongezeka kwa migawanyiko miongoni mwa Wakenya, Bw Odinga aliwakosoa wapinzani ambao aliwataja kuwa ‘manabii wa maangamizi’, akiwashutumu kwa kutumia changamoto zilizopo kueneza hali ya kukata tamaa kwa Wakenya.

“Kwa wakati huu, wengi wenu mnajiuliza ikiwa mtaweza kujikimu baada ya kuondoka hapa kwa sababu ya jumbe kutoka kwa manabii wabaya. Nchi imejaa manabii wa maangamizi na huzuni, wanaume na wanawake wanaohimiza watu kukubali kukata tamaa kama njia ya maisha,” alisema.

Alizungumza wakati wa hafla ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha Kabarak, Nakuru. Mapema mwezi huu,Rais Ruto alisema pepo mbaya inaenea nchini Kenya, ikilenga kupinga mipango inayoendeshwa na serikali

“Kuna pepo mbaya ya kupinga kila kitu miongoni mwetu. Kutoka kwa muundo mpya wa ufadhili wa Chuo Kikuu, Makazi ya bei nafuu, kampeni ya kitaifa ya chanjo ya mifugo pamoja na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). Pepo mbaya imefikia hatua ya kupinga michango inayotolewa kwa makanisa. Roho ya kupinga kila kitu,” Ruto aliambia hadhira kwa Kiswahili.

“Tuiombee nchi yetu, na tuondoe roho hii ya kupinga kila kitu kwenye mtandao’ Rais Ruto alisema wakati huo.Katika hotuba yake mjini Kabarak, Bw Odinga aliangazia changamoto nyingi zinazokabili taifa, zikiwemo ukosefu wa ajira na mabadiliko ya hali ya hewa kuwa tishio kubwa kwa umoja wa kitaifa.

Bw Odinga alibainisha kuwa matatizo ya kiuchumi yameifanya nchi kuwa katika hali mbaya ambapo wananchi wanazidi kupoteza imani na taasisi za serikali.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA