Siasa

Raila atakuwa rais wa tano wa Kenya – Wabunge

December 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JUSTUS OCHIENG

CHAMA cha ODM, sasa kinawataka Wakenya kuanza kujiandaa kwa utawala wa kiongozi wao, Raila Odinga baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Maafisa wa chama hicho wanasema kwamba, Bw Odinga atakuwa rais wa tano wa Kenya ingawa Waziri Mkuu huyo wa zamani bado hajatangaza kugombea urais.

Ingawa umaarufu wa chama hicho ulitiliwa shaka baada ya mgombea wake kubwagwa kwenye uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge cha Msambweni, wafuasi wake wanasisitiza kingali maarufu na Bw odinga ataibuka mshindi wa urais kwenye uchaguzi wa 2022.

Wanasikitika kuwa Bw Odinga amechelewa kutangaza nia yake ili Wakenya waanze kujiandaa kwa utawala wake. Kwa sasa, Bw Odinga anaendelea kupanga mikakati yake akipalilia umaarufu katika eneo la Mlima Kenya.

Mwishoni mwa wiki, wazee wa jamii ya Waluo waliandamana na baadhi ya washirika wake wa kisiasa kukutana na wazee wa eneo la Mlima Kenya katika Kaunti ya Nyeri kabla ya watu mashuhuri kaunti ya Muranga kumtembelea nyumbani kwake Bondo.

Inasemekana mikutano hiyo miwili ilikuwa ya kuandaa ziara ya Bw Odinga katika Mlima Kenya. Jumapili, mwekahazina wa chama cha ODM, Timothy Bosire alisema kwamba, Wakenya hawana budi kukumbatia utawala wa Bw Odinga kama rais wa tano wa Kenya.

“Kwa kufahamu hali ya kisiasa nchini ikizingatiwa haja ya umoja wa kitaifa na kufufua uchumi kwa lengo la kuafikia ndoto za mababu wetu, Wakenya wanafaa kujiandaa kwa Bw Odinga kuwa rais wa tano wa Kenya,” Bw Bosire aliambia Taifa Leo.

Bw Odinga amekanusha kwamba BBI ni ya kumwezesha kuingia Ikulu kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mwaka 2019, kakake Raila, Oburu Oginga alisema kwamba lengo la BBI ni kumfungulia kiongozi wa ODM milango ya kuingia Ikulu.

“Watu watulie kwa sababu hatujajiondoa kwenye uchaguzi wa 2022. Hatuoni anayeweza kumshinda Raila na ndio maana tunasema anafaa kuwa rais hata kwa muhula mmoja,” Bw Oginga alisema.

Mbunge wa Uriri, Mark Nyamita alisema Raila hana budi kuwa rais wa tano wa Kenya.