Siasa

Ruto ateka makao makuu ya Jubilee

October 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto Alhamisi aliongoza wabunge 32 washirika wake wa kisiasa kuteka makao makuu ya chama cha Jubilee kwa saa sita na kuyatumia kufanya mkutano.

Dkt Ruto aliwasili katika ofisi hizo zilizoko Pangani jijini Nairobi mwendo wa saa tatu asubuhi bila kutarajiwa, na kukutana faraghani na wabunge na maseneta wa mrengo wa Tangatanga, ambao wamekuwa wakilaumu maafisa wakuu wa chama kwa usimamizi mbaya na ubaguzi.

Duru zilisema kwamba maafisa wa chama hicho akiwemo Katibu Mkuu Raphael Tuju hawakuwa na habari kuhusu mkutano huo uliochukua takriban saa sita au ajenda zake.

Wanahabari walifungiwa nje ya ofisi hizo huku walinzi wakisema walikuwa na maagizo kutowaruhusu ndani.Kuanzia saa tatu, Dkt Ruto na washirika wake walitawala ofisi hizo na hakuna aliyefahamu walichokuwa wakifanya au kujadili.

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe, alitaja tukio hilo kama jaribio la mapinduzi kwa kuwa lilifanyika wakati Rais Uhuru Kenyatta, ambaye ni kiongozi wa Jubilee, yuko nje ya nchi.

“Kwa nini Ruto alisubiri Rais Uhuru Kenyatta akazuru Ufaransa ili atawale ofisi za Jubilee kana kwamba ni kiongozi wake? Ruto anataka kufanya mapinduzi katika chama cha Jubilee,” akasema Bw Murathe.

Rais Kenyatta yuko katika ziara rasmi nchini Ufaransa.Ingawa Dkt Ruto ni Naibu Kiongozi wa Jubilee, washirika wake wamekuwa wakilalamika kwamba ametengwa katika masuala ya uongozi wa chama hicho wakimlaumu Bw Tuju kwa usimamizi mbaya na matumizi mabaya ya pesa.

Wiki iliyopita, juhudi za Dkt Ruto kutaka chama hicho kusimamisha mgombeaji kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Msambweni, Kaunti ya Kwale zilizimwa na Bw Tuju aliyesema kwamba waliamua kutoshiriki uchaguzi huo.

Dkt Ruto alivamia ofisi hizo siku mbili mfululizo kabla ya kuzimwa na tangazo la Bw Tuju lililoidhinishwa na Rais Kenyatta ambaye alikuwa Mombasa wakati huo.

Kulingana na Bw Murathe, Bw Tuju na Mkurugenzi Mkuu wa Jubilee James Waweru hawakuwa na habari kuhusu mkutano wa jana wa Dkt Ruto na washirika wake.

“Badala ya kuendeleza shughuli za serikali kama naibu rais wakati rais yuko nje ya nchi, ameamua kujihusisha na masuala ya chama,” alisema Bw Murathe.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa chama hicho, Albert Memusi pia alithibitisha kwamba hakuwa na habari kuhusu ajenda za mkutano huo.Baada ya kukutana kwa saa sita, Dkt Ruto aliondoka bila kuhutubia wanahabari ilivyo kawaida yake.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge waliokutana naye walikanusha kwamba walilenga kupindua uongozi wa chama.Seneta wa Meru Mithika Linturi alisema walikuwa katika ofisi hizo kuuliza maswali kwa niaba ya wapigakura.

“Hakukuwa na mapinduzi. Unawezaje kufanya mapinduzi katika nyumba yako? Chama cha Jubilee ni chama chetu na hakuna mapinduzi,” alisema Bw Linturi.

Alisema kwamba kama wanachama wa chama tawala wana haki ya kushauriana kuhusu masuala yanayoathiri nchi.“Wakenya wanataka kujua mipango ya chama. Isipokuwa rais na viti vingine vichache, chama hakijafanya uchaguzi mwingine,” aliongeza Bw Linturi.

Wanatangatanga wamekuwa wakimlaumu Bw Tuju kwa kuchelewesha uchaguzi wa mashinani wa chama hicho. Vilevile, wamekuwa wakidai kwamba Bw Tuju amekuwa akiwawekea vikwazo wasishiriki uchaguzi huo ambao ulipaswa kufanyika Machi, lakini ukaahirishwa kufuatia janga la corona.

Mbunge wa Kandara, Alice Wahome, ambaye pia alihudhuria mkutano wa jana alisema kwamba mrengo wa Tangatanga ni sehemu ya Jubilee, na madai kwamba walinuia kufanya mapinduzi ni ya kupotosha.