• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
Serikali yatakiwa kusaka mabaki  ya Kimathi, Samoei na Menza

Serikali yatakiwa kusaka mabaki ya Kimathi, Samoei na Menza

Na MWANGI MUIRURI

MASHUJAA wa vita vya ukombozi (Mau Mau) sasa wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta aifanye mada kuu ya kiserikali kusaka mabaki ya mashujaa Dedan Kimathi na Koitalel Arap Samoei waliouawa na utawala wa kikoloni na kisha yapewe utambuzi na mazishi ya kitaifa.

Wamemtaka Rais Kenyatta awatuze jibu la ufanisi kabla atoke afisini mwishoni mwa mwaka wa 2013.

Pia, wamemtaka awaelezee mikakati yake ya kuwatuza manusura walio hai wa vita hivyo vya ukombozi dhidi ya ukoloni katika taifa hili.

Huku mabaki ya Bw Kimathi aliyenyongwa miaka 62 iliyopita na serikali hiyo ya Kikoloni yakiwa hayajajulikana yalipo hadi sasa, kichwa cha Bw Samoei aliyekuwa mpiganiaji uhuru wa jamii ya Nandi huaminika kuwa kimehifadhiwa katika makavazi ya kivita nchini Uingereza.

Mwenyekiti wa Kenya African Mau Mau Union (KAMMU) Bw Hackman Muniu pia alimtaka Rais Kenyatta amtawaze marehemu Bi Mekatilili Menza wa jamii ya Giriama na ambaye pia alishiriki harakati za ukombozi kikamilifu hadhi ya mwanamke shujaa wa kitaifa.

“Ni jambo la busara mwanamke huyo wa kipekee atambuliwe sawasawa katika Uhuru wetu na pia Kichwa cha Samoei kirejeshwe hapa nchini na kuzikwa kishujaa,” asema Bw Muniu.

Bw Samoei aliuawa na wakoloni mwaka wa 1905 kufuatia miaka 10 ya juhudi zake za kuongoza jamii yake kukaidi utawala huo haswa katika ujenzi wa mtandao wa reli kutoka Kenya hadi Uganda.

Aliuawa kwa kupigwa risasi na kisha kichwa chake kikakatwa na Wakoloni ambao hatimaye walikihamishia hadi Nchini Uingereza kama Ishara ya ushidi wa kivita.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa eneo la Mlima Kenya Mzee Jotham Kiama, mashujaa hao wanateta kuwa kuwa taifa hili linachelewa katika juhudi za kusaka mabaki ya marehemu Kimathi kwa kuwa wanaoweza kusaidia katika harakati hizo wamezeeka pakubwa kiasi cha kupoteza umakinifu wa kimawazo.

Marehemu Kimathi alinyongwa masaa ya asubuhi mnamo Februari 18, 1957 baada ya kuhukumiwa na jaji Mkuu wa Kikoloni Kenneth O’Connor kwa madai ya kupatikana na silaha na pia kuendeleza vita dhidi ya serikali ya kikoloni.

Wanashikilia kuwa rais Kenyatta kama mtoto wa mwanzilishi wa taifa hili ako na deni lao la miaka hiyo yote ambapo serikali tangulizi zimekuwa zikizembea au kukosa umuhimu wowote wa harakati za kuwatambua kitaifa mashujaa hao wenda zao kama njia moja ya kuhifadhi historia ya ukombozi kwa uzito.

Ni hivi majuzi tu Wakili Paul Muite alinukuliwa akisema utafiti wake umeonyesha kuwa mabaki ya Kimathi hayakuzikwa, mbali yalichomwa ama yakaangamizwa kwa kemikali na wakoloni hivyo basi kuondoa matumaini ya kuwahi kupewa mazishi ya kitaifa.

Matakwa mengine yanayotolewa na manusura hao wa vita vya ukombozi ni kutwaliwa kwa mashamba ambayo yanamilikiwa na mabwanyenye ambao hawayatumii na yapewe wasio na mashamba hapa nchini.

Aidha, wanaitaka serikali itenge hazina ya mashujaa ambayo itawasaidia waliosalia kujiendeleza kimaisha.

Mashujaa hao wanalalamika kuwa hakuna wanahistoria ambao wamejitokeza kuandikia vizazi historia ya kutegemewa kuhusu mashujaa na harakati zao katika kutafuta utaifa tulio nao kwa sasa.

Matakwa mengine ambayo yamekuwa yakichipuka katika harakati zao za kusaka utambuzi ni watengewe nyadhifa za kitaifa za kutoa ushauuri kwa serikali kuu na pia zile za Kaunti na pia washirikishwe kikamilifu katika harakati za kurejesha na kuhifadhi tamaduni za kijamii hapa nchini.

You can share this post!

‘Aliyemzika’ Dedan Kimathi asimulia shujaa...

Tovuti 18 za serikali zadukuliwa

adminleo