Simba Arati-ODM haitacheka na wanaokiuka haki za Wakenya
NAIBU kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Gavana Simba Arati, amesema chama hicho kitaendelea kuiwajibisha serikali licha ya kuiunga mkono.
Akizungumza mjini Nakuru wakati wa ziara yake, Bw Arati alisema chama cha ODM kitasimama imara kutetea misingi ya aliyekuwa kiongozi wa chama hicho, hayati Raila Odinga, ikiwemo demokrasia, usawa na uongozi bora.
“Hata kama tupo katika serikali jumuishi, hatutafumbia macho ukiukaji wa haki za binadamu na matumizi mabaya ya mamlaka. Kama chama cha ODM, kuna watu ambao hatutakuwa tukicheka nao kuhusu mustakabali wa nchi hii,” alisema Bw. Arati.
Gavana huyo wa Kisii alisisitiza kuwa ODM itaendelea kutekeleza makubaliano ya ushirikiano yaliyosainiwa kati yake na serikali hadi mwaka 2027, baada ya hapo kila upande utaamua mwelekeo wake wa kisiasa.
Bw Arati alieleza kutoridhishwa na baadhi ya vitendo vya serikali ya sasa akisema vinakinzana na maadili na misingi aliyosimamia Bw Odinga wakati wa uhai wake.
Kwa mujibu wa Arati, chama hicho hakiungi mkono kile alichotaja kama wizi wa mali ya umma, mauaji ya kiholela, matumizi mabaya ya mamlaka na ukiukaji wa haki za binadamu.
“Baba ameondoka, lakini ametuachia makamanda wa kutosha wa kuendeleza mapambano ya ukombozi wa nchi hii. Sote tumeshuhudia mauaji ya kiholela, matumizi mabaya ya mamlaka na uporaji wa mali ya umma. Natoa wito kwa Wakenya wote, hasa vijana, kulinda taifa hili kwa gharama yoyote ile,” alisema.
Alikumbuka tukio la mwaka 2023 ambapo alisema serikali ilituma maafisa wa GSU katika ofisi yake kumtisha, akisema hiyo ilikuwa dalili ya jinsi baadhi ya maafisa wa serikali wanavyokiuka sheria na kutumia nguvu vibaya.
Kauli ya Arati inajiri huku chama cha ODM kikiwa katika hali ya taharuki kufuatia kifo cha Bw Odinga.
Inadaiwa Bw Arati ni miongoni mwa kundi linaloongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, wanaotaka chama kiendelee kuwa na msimamo huru kukosoa serikali.
Kundi jingine linalounga mkono kuendelea kwa ushirikiano wa ODM na serikali linaongozwa na Mwenyekiti wa chama Gladys Wanga, pamoja na Mawaziri John Mbadi, Hassan Joho na Opiyo Wandayi.
Ziara ya Bw Arati mjini Nakuru ilivutia umati mkubwa, na kusababisha shughuli katika barabara kuu za jiji hilo kusimama kwa muda.
Gavana huyo alisema yuko ana jukumu la kuunganisha wanachama wa ODM kufuatia kifo cha Bw Odinga, akisisitiza kuwa chama hicho kitahakikisha kinadumisha ngome zake za jadi na kupanua wigo wake kisiasa.
“ODM bado ni chama imara. Tutahakikisha tunalinda ngome zetu za kisiasa na kuendeleza maono ya Baba kwa vizazi vijavyo,” alisema.