Sonko aelekea ‘kichinjioni’ hoja ikipita
Na COLLINS OMULO
MADIWANI wa Kaunti ya Nairobi wameanza rasmi mchakato mpya wa kumng’oa Gavana Mike Sonko mamlakani.
Hii ni baada ya madiwani 86 kutia saini ilani ya kuwasilisha hoja ya kumtimua gavana huyo anayekumbwa na matatizo tele katika uongozi wake. Sahihi 42 pekee ndizo zilizohitajika.
Akitaja hoja hiyo, Kiongozi wa Wachache katika bunge la kaunti, Bw Michael Ogada, aliwasilisha sababu mbalimbali za dhamira ya kumng’oa Sonko mamlakani.
Miongoni mwa sababu hizo ni madai ya kukiuka katiba, utumizi mbaya wa mamlaka, utendaji wa uhalifu chini ya sheria ya kitaifa na kimataifa, na kukosa uwezo wa kimwili na kiakili kuendesha shughuli za serikali za kaunti inavyofaa.
Bw Ogada alisema wiki ijayo, atawasilisha ushahidi wa kutetea sababu alizotoa huku akisisitiza kuwa Gavana ameshindwa hata kutekeleza majukumu aliyobakishiwa baada ya kukabidhi mengine kwa Serikali Kuu.
“Hatutaendelea kukaa tukisubiri milele. Wakati sasa umefika na madiwani wa Nairobi tumeamua lazima tuchukue hatua na kuhakikisha hali ya kawaida inarudishwa jijini,” akasema diwani huyo wa Embakasi.
Aliongeza, “Hatua pekee tunayoweza kuchukua kama madiwani ni kumtimua aende nyumbani ili wananchi wachague gavana mwingine na tusonge mbele. Wakazi lazima wahudumiwe.”
Kwa upande wake, kiranja wa wachache katika bunge hilo, Bw Peter Imwatok alisema Spika Benson Mutura atamkabidhi gavana notisi hiyo inayoeleza sababu za madiwani kutaka aondolewe mamlakani.
Baadaye Sonko atapewa siku saba kuwasilisha utetezi wake kabla ya hoja rasmi ya kumtimua ipelekwe katika bunge hilo.
“Kufikia Alhamisi ijayo, madiwani watatoa uamuzi wao na sioni kama watakuwa na uamuzi mwingine ila kumtuma akajitetee mbele ya Seneti,” akasema Bw Imwatok.
Hii ni mara ya pili kwa madiwani kujaribu kumng’oa mamlakani gavana huyo.
Jaribio la kwanza mnamo Februari lilitibuka wakati Rais Uhuru Kenyatta alipoingilia kati.
Hoja ya kumtimua ikipitishwa na madiwani 82 kati ya 122 wa Nairobi, Spika Mutura atatakikana kumjulisha Spika wa Seneti kuhusu uamuzi wa madiwani kabla siku mbili zikamilike.
Katika siku za hivi majuzi, Sonko amekuwa akimshambulia wazi Rais Kenyatta katika mitandao ya kijamii, pamoja na Mkuu wa Idara ya Huduma za Nairobi (NMS) Jenerali Mohamed Badi.