Siasa

Wabunge waliounga Gachagua kutemwa waanza kuzomewa kwenye mikutano ya hadhara

Na MWANGI MUIRURI November 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WABUNGE kutoka eneo la Kati mwa Kenya waliomsaidia Rais William Ruto kutimiza ajenda yake ya kumtimua aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua, sasa wanakabiliwa na wakati mgumu katika maeneo bunge yao.

Wakazi wa maeneo hayo wanawashambulia kwa maneno kwa kuunga mkono kutimuliwa kwa Bw Gachagua na nafasi yake kupewa Profesa Kithure Kindiki.

Kwa upande wake, Bw Gachagua amewataka wafuasi wake kuwaadhibu wabunge hao aliowataja kama wasaliti kwa kukaidi msimamo wa wapiga kura na kuunga mkono hoja ya kumwondoa afisini iliyodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Bw Mwengi Mutuse.

Hali hii huenda ikaathiri nafasi ya wabunge hao kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Mnamo Jumatatu, Mbunge wa Nyeri Mjini, Bw Dancan Mathenge, alikabiliwa na wakazi wenye hasira waliomzomea vikali wakimtaja kama “msaliti”.

Alishindwa kabisa kuwahutubia wakazi hao hali iliyomlazimu kuondoka eneo hilo haraka baada ya idadi ya watu waliokuwa wakimzomea kuongezeka.

Hili sio tukio la kipekee kwa kuwa wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya waliomsaidia Rais Ruto kumtimua Bw Gachagua wanapitia wakati mgumu kwa kushambuliwa kwa maneno kila mara katika maeneo ya umma na kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Juzi, wazee sita walikutana katika kaunti ndogo ya Kigumo na kuamua hadharani kumlaani Mbunge Mwakilishi wa Murang’a, Bi Betty Maina ambaye ni hasidi mkubwa wa Bw Gachagua.

Wakiongozwa na Mzee Mungai Njama, wazee hao walifanya matambiko ambapo walivunja vibuyu, nyungu na njele wakiapa kuwa mustakabali wa kisiasa wa Bi Maina utasambaratika.

Lakini Bi Maina alijibu kwa kusema hivi: “Wale waliowalipa pesa wazee ndipo wanilaani wataishia kujilaani wao wenyewe.”

Ili kuzuia kushambuliwa kila mara kupitia mitandao ya kujamii, Mwenyekiti wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Bi Cecily Mbarire, ameamua kuzima sehemu ya maoni katika akaunti zake za mitandao ya kujamii.

Msururu huu wa mashambulio dhidi ya wanasiasa wa Mlima Kenya ambao walimsaliti Bw Gachagua hautakoma hivi karibuni, kulingana na Mbunge wa zamani wa Bahati, Bw Kimani Ngunjiri.

“Viongozi wanapaswa kuheshimu maoni na misimamo ya wapiga kura. Hitaji la ushirikishaji wa maoni kutoka kwa wananchi ni la kikatiba na linafaa kuheshimiwa,” anaongeza.

Bw Ngunjiri anakumbuka kisa cha Oktoba 11, 2024, siku tatu baada ya Bunge la Kitaifa kupitisha hoja ya kumtimua Bw Gachagua, wabunge wandani wa Rais Ruto walizomewa katika hafla ya mazishi katika eneo bunge la Bahati.

Mazishi hayo ya kakake mbunge wa eneo hilo, Bi Irene Njoki, Henry Gachie, yaligeuzwa kuwa jukwaa la kutoa kauli za kuipinga serikali ya Kenya Kwanza.

Ilimlazimu Gavana wa Nakuru, Bi Susan Kihika kunyenyekea na kuwaomba waombolezaji wamruhusu kusoma risala za rambirambi kutoka kwa Rais Ruto.

Lakini wabunge walioandamana naye walizimwa kabisa kuwatuhutubia waomboleza walioonekana kukerwa na hatua yao ya kuuunga mkono hoja ya kumtimua Gachagua.

Waliozimwa kuzungumza ni pamoja na Mbunge wa Ndia George Kariuki, Sabina Chege (Mbunge Maalum), Anne Wamuratha (Mbunge Mwakilishi wa Kiambu), Rahab Mukami (Mbunge Mwakilishi wa Nyeri).

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi ambaye pia alikatazwa kuzungumza, baadaye aliwalaumu watu fulani, ambao hakuwataja majina, kwa kuwalipa waombolezaji wawazomee.