Makala

Sifa spesheli za pweza zinazofanya wavuvi kumng’ang’ania

June 5th, 2024 4 min read

NA KALUME KAZUNGU

MBALI na nyama ya pweza kusifiwa kuwa na virutubisho vingi, sifa kwamba supu ya pweza husaidia wanaume kuimarisha nguvu za kiume humfanya pweza kutafutwa kama dhahabu na wavuvi baharini.

Wahenga wakanena….“Umekuwa pweza wajipalia makaa.”

Ni methali inayotokana na sifa au tabia za mnyama pweza wakati anapochomwa kwenye makaa ili kufikishwa mezani kama kitoweo.

Hapa, mnyama huyu hujikunjakunja, kujipindapinda au kujipetapeta wakati anapoivishwa kwenye meko motoni.

Mvuvi akiwa amewashika pweza. PICHA | KALUME KAZUNGU

Ikumbukwe kuwa pweza ni mnyama wa baharini mwenye umbo la duara lililozungukwa na mikono au minyiri minane mirefu.

Ni hiyo mikono au minyiri ambayo hukunjana au kupindanapindana wakati pweza anapowekwa au kukaushwa kwenye makaa kiasi kwamba waja wakailinganisha hali hiyo na kujigeuzageuza, hivyo ‘kujipalia makaa.’

Ni mnyama ambaye siyo rahisi kupatikana baharini.

Wavuvi wanaofaulu kumnasa hupitia jazba nyingi hadi kufikia kiwango hicho.

Bw Ali Mzee, 45, mvuvi wa kisiwa cha Lamu ambaye amefanya kazi ya uvuvi wa pweza kwa karibu miaka 20 sasa, anakiri kuwa kazi ya kumtafuta pweza ni ngumu sana.

Bw Mzee anafafanua kuwa mtu au mvuvi huhitaji kuwa na ujuzi maalum, afya iliyo dhabiti na pia awe ni mwenye kujihami na vifaa vinavyostahili kuitekeleza kazi hiyo ya kumvua pweza kikamilifu.

Anataja tabia za kiajabuajabu za pweza, ikiwemo kujibadilisha rangi kulingana na sehemu aliyopo kuwa miongoni mwa vigezo vinavyoifanya kazi ya kumvua mnyama huyo kuwa ngumu na ya kuchosha.

Isitoshe, pweza mara nyingi huwa na damu ya rangi ya bluu (samawati) ambayo ina madini ya kopa kwa jina hymocianin ambayo huwasaidia wanyama hao kuishi chini au kwenye sakafu ya bahari.

Maji yanapokusanyika kwa wingi mahali pamoja, kwa mfano baharini, hutwaa rangi ya ulimwengu ambayo ni ya bluu.

Hilo linaashiria wazi jinsi rangi ya pweza inavyomsaidia kujificha kwenye mazingira ya ndani ya bahari, hivyo kumpa kibarua cha mwaka mvuvi kumsaka na kumnasa mnyama huyo.

“Kwa kweli kutafuta pweza majini sio rahisi. Ni kiumbe wa ajabu ambaye hata unaweza kumpita na usimuone. Baadaye ukimchunguza kwa makini unamuona palepale kwani hujibadilisha kwa rangi tofauti kulingana na sehemu aliyomo kwa wakati ule,” akafafanua Bw Mzee.

Lakini je, ni sifa gani spesheli za huyo mnyama pweza ambazo kila kukicha zinawafanya wavuvi, hasa eneo la Pwani ya Bahari Hindi, kumng’ang’ania licha ya dhiki wanazopitia katika kumtafuta hadi kumnasa?

Kwanza nyama na supu ya pweza ni tamu.

Ila utamu wa kitoweo cha pweza hutegemea sana matayarisho yanayofanywa kipindi baada ya kumvua.

Bi Nana Nadhiru, mpishi mashuhuri wa pweza na vyakula vingine vya baharini katika kisiwa cha Pate, Lamu Mashariki, anasema pweza lazima aandaliwe kwa ustadi sana.

“Ni kweli nyama ya pweza ina utamu wake ila huenda ukaupoteza utamu huo endapo utakosea hatua moja katika kumtayarisha. Licha ya kwamba huwa yuko katika hali oevuoevu akiwa mbichi, pweza anafaa kuwa mgumu baada ya kupikwa,” anaeleza Bi Nadhiru.

Bi Nadhiru anafafanua kuwa kumpondaponda pweza ili alainike ni miongoni mwa hatua za kwanzakwanza za maandalizi.

Mbali na nyama tamu, pweza pia hutayarishwa kupitia kumchemsha kwa muda, hivyo kuipata supu au mchuzi wake.

Wapishi au waandalizi wengine wa mnyama huyo huongeza viungo na ladha nyingine kama vile limau, ndimu au hata nazi kwenye supu au mchuzi wa pweza.

Pweza na supu yake pia vina sifa muhimu na spesheli ambazo pia zimewasukuma wavuvi kumtafuta kila siku na kumvua ikizingatiwa kuwa hata soko au uhitaji mahotelini na majumbani uko juu.

Sifa hiyo ni ile ya imani kuwa anaongeza nguvu za kiume.

Bw Kassim Shee, 74, mzee wa Kizingitini, Lamu Mashariki, anasema katika utamaduni, hasa wa Wapwani, supu ya pweza imekuwa ikipendwa na wanaume, hasa wale wa umri wa uzeeni, wakijua fika kuwa ni jeki kimpango.

“Supu ya pweza si supu tu ya kawaida kama zile nyingine ambazo mja anazitambua au kuwahi kunywa. Hapa utakunywa supu ya pweza na kisha kujihisi damu ikiamka. Yaani hii supu ya pweza inasaidia kupiga jeki nguvu za kiume,” akasema Bw Shee huku akicheka kuashiria kuridhishwa na mchango wake huo.

Hassan Abdalla, ambaye pia ni shabiki wa mlo wa pweza na kunywa supu, anasema kitoweo hicho, hasa supu, huwa hakikosi mezani kwake kila jioni kwani humpa msisimko wa mwili wa aina yake.

Pweza na supu yake pia ni chakula cha kitamaduni kinachopendwa na kuenziwa tangu jadi, wataalamu wa lishe na afya pia wakitaja manufaa tele ya kitoweo hicho.

Duncan Mwatela, ambaye ni afisa binafsi wa masuala ya lishe Lamu, anasisitiza kuwa pweza ni chakula muhimu kwa afya na lishe ya mwanadamu.

Bw Mwatela anasema pweza ana virutubisho vingi.

Kirutubisho au kirutubishi ni kiini kinachopatikana katika chakula ambacho huwezesha viumbe kukua.

Yaani ni kiini kwenye chakula kinachofanya mwili wa binadamu kuwa na nguvu, joto na kuweza kukua.

“Ni bayana kwamba pweza huwa ana madini joto (iodine). Madini haya husaidia sana katika masuala ya uzazi, iwe ni kwa mwanamke au mwanamume. Isitoshe, pweza ana utajiri mwingi wa protini,” akasema Bw Mwatela.

Daktari Mshauri wa Kituo cha Afya cha Bluenile Mkoroshoni, Kaunti ya Kilifi, Duncan Amani Chai naye anataja kuwepo kwa ukwasi wa protini katika pweza kuwa muhimu kwani huwasaidia walaji kujenga mwili na kuweka kinga mwilini, hivyo kujikinga na aina mbali mbali za saratani.

“Ulaji wa pweza hata husaidia huongeza damu mwilini kutokana na chembechembe nyekundu za damu anayoitoa mnyama huyo,” akasema Dkt Chai.

Sifa nyingine ya kufurahisha na kuridhisha nafsi zaidi ni kwamba pweza hana madhara yoyote ya kiafya kwa binadamu.

Kuna washauri wengine wa lishe ambao hata wamekuwa wakiwahimiza kina mama wanaonyonyesha na ambao hawana maziwa ya kutosha kwa watoto wao kujitahidi kunywa supu ya pweza.

Wanasema supu ya pweza inaweza kuongeza kiwango cha maziwa ya mama kwa wingi kutokana na virutubisho vilivyoko vya protini na madini ya chuma.