Habari Mseto

Sijawahi kukutana na Linturi wala kufanya kazi naye – Daktari Karanja

Na FRIDAH OKACHI August 2nd, 2024 1 min read

WAZIRI mteule katika Wizara ya Kilimo na Mifugo Daktari Mwihia Karanja, alikana kufanya kazi kama msaidizi wa Waziri wa zamani Bw Mithika Linturi.

Madai hayo yalisambaa kwenye mitandao ya kijamii Julai 19, 2024 punde tu alipotangazwa na Rais William Ruto kuchukua nafasi ya kuwa Waziri wa Kilimo.

Akiwa mbele ya Kamati Maalum kwa mahojiano Ijumaa, Agosti 2, 2024, Bw Karanja, alieleza kushangazwa na madai hayo.

Alisisistiza kibinafsi au kitaaluma hajawahi hata kukutana na waziri huyo wa zamani.

Hii ni baada ya Kiongozi wa Wengi kwenye Bunge la Kitaifa na Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah kumtaka kufafanua zaidi mahusiano yake na waziri wa zamani kwenye wizara hiyo.

“Kuwa msaidizi wake, hilo lilinishangaza sana. Nikiwa mbele ya Kamati hii, sijawahi kukutana na waziri huyo na sijawahi kuwa msaidizi wake wa kibinafsi,” akasema Dkt Karanja.

Kwenye mahojiano hayo, suala la ufisadi lilijitokeza huku Mbunge wa Suna Mashariki akimuonya huenda akafutwa kazi baada ya mwaka mmoja kutokana na ufisadi uliokithiri kwenye Wizara hiyo kutokana na wafanyabiashara wafisadi.

Mbunge huyo alisema wafisadi hao wamezingira afisi za serikali na kutekeleza uhalifu bila kuchukuliwa hatua.

Bw Junet alimuonya Daktari Karanja, iwapo hatakuwa mwangalifu na kukosa kuchukua hatua kwa wafisadi hao, basi huenda wembe uliompata Waziri wa zamani Mithika Linturi utamkata.

Kwa upande wake Daktari Karanja alihakikishia mbunge huyo na Wakenya, iwapo ataidhinishwa na kamati hiyo kwenye wadhifa huo, basi atafanya kwa juhudi zake kuwaondoa wafanyabiashara hao.

“Najua suala la wafanyabiashara wafisadi ni shida kubwa na kuna njia mbalimbali nitakazotumia. Iwapo nitaidhinishwa na kamati hii, basi nawapa notisi wafisadi hao. Notisi hiyo ni kuwafahamisha kuondoka kwenye biashara hiyo, kulingana na kanuni ambazo ninaziheshimu sana, sitakubali kuhujumiwa,” alisema waziri huyo mteule.