Makala

Sikuolewa na Mzee Kibor sababu ya mali bali mapenzi ya dhati, asema mjane Eunitah

May 10th, 2024 1 min read

NA TITUS OMINDE

MKE wa nne wa marehemu Jackson Kibor, Eunitah Kibor, 45, ametupilia mbali madai kuwa aliamua kuolewa na mwendazake kwa sababu ya mali.

Mwanamke huyo aliyeolewa na marehemu mnamo 2002 anasema kuwa alikuwa na mapenzi ya dhati na Mzee Kibor.

Bi Eunitah alisema bado anampenda marehemu Mzee Kibor na kwamba hana mpango wa kuolewa tena.

Akizungumza na Taifa Leo mjini Eldoret, mwanamke huyo alikanusha madai kuwa nia yake kuolewa na marehemu ilikuwa ni kujilimbikizia mali.

“Mzee Kibor alinipenda sana na ndiye alikuwa akiniwinda. Kando na hayo, mimi sikuja hapa kwa sababu ya mali,” alisema Bi Eunitah.

Pia alikanusha madai kuwa yeye ndiye aliyemfanya Mzee Kibor kwenda kortini kuwataliki wake zake wengine.

Mzee Jackson Kibor ambaye sasa ni marehemu. Picha|Maktaba

“Niliolewa na Mzee Kibor mwaka 2002. Tumejaliwa watoto watano na hadi kifo chake tulikuwa tunapendana kwa dhati. Hakuna mwanaume mwingine duniani ambaye anaweza kunipa mapenzi niliyokuwa nikipata kutoka kwa Mzee Kibor,” akasema Bi Eunitah.

Baada ya kifo cha Mzee Kibor mnamo 2022, Bi Eunitah alijikuta katika vita na watoto wa marehemu kuhusu ugavi wa mali.

Bi Eunitah ambaye alimshutumu mwana mkubwa wa Kibor Philip Kibor kwa kukosa heshima kwake amesema yuko tayari kuelewana na wana wa marehemu jinsi ya kugawa mali ya familia akisisitiza kwamba mazungumzo kuhusu mali hiyo lazima yalingane na wosia wa Mzee Kibor.

Mzee Kibor, mkulima maarufu kutoka Uasin Gishu aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 88.

Watoto 27 wa wajane wawili wa marehemu wamekuwa wakipiga wosia ambao Bi Eunitah, anadai kuwa ni hati ya kweli ambayo tajiri huyo aliiacha kama mwongozo na matakwa yake kuhusu namna utajiri wake unapaswa kugawanywa.

Familia ya marehemu imezama katika vita kuhusu usimamizi na ugavi wa mali ya marehemu Kibor inayokadiriwa kuwa zaidi ya Sh16 bilioni na kuenea Uasin Gishu, Trans-Nzoia, Nakuru, Nairobi na Mombasa.