Habari za Kaunti

Simba wageuka sinema ya bure kwa wasafiri barabarani

January 27th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

BAADHI ya wasafiri waliokuwa wakielekea mjini Nyeri kutoka Nyahururu, Jumatano usiku walilazimika kukatiza safari yao kwa muda, kutazama sinema ya bure ambapo simba kadhaa waliokuwa wametoka mbugani walionekana wakiwa wamelala barabarani.

Simba hao walikuwa wametokea katika shamba la Solio, kilomita chache kutoka kituo cha kibiashara cha Wiyumiririe.

Shamba hilo kubwa linapakana na msitu wa Aberdares.

Kulingana na wasafiri waliozungumza na Taifa Leo, simba hao hawakuonekana kuwa tishio kwao, kwani baadh yao walikuwa wamelala.

“Inaonekana walikuwa kwenye safari ndipo wakaamua kupumzika kwa muda kandokando mwa barabara,” akasema Bw James Murugu, dereva wa mojawapo ya matatu zilizolazimika kusimama ili kuwapa abiria wake nafasi ya kipekee kuwaona simba.

“Baadhi yao walinirai kusimamisha gari ili kuwapa nafasi ya kuwaona wanyama hao,” akasema Bw Murugu.

Kulingana na Bi Mary Nyaruai, ambaye alikuwa miongoni mwa abiria hao, hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kuwaona simba moja kwa moja.

“Ingawa ni wanyama hatari, hii ni mara ya kwanza kuwaona wakiwa karibu hivi. Ni tukio la kipekee!” akasema.

Ijapokuwa hakuna makazi ya watu yaliyo karibu na eneo hilo, tukio hilo limezua wasiwasi kwamba, huenda kuna wanyamapori wanaovuka nyua za stima zilizowekwa katika mbuga zao na kuvuka katika maeneo ya raia.

Eneo hilo linapakana na mbuga za wanyama za Aberdares na Mlima Kenya.

Wakazi wa maeneo jirani kama Nairutia, Mahiga Meeru kati ya mengine, hata hivyo, wamekuwa wakilalamikia uvamizi wa wanyamapori kama chui na fisi dhidi ya mifugo wao.

Hadi tukienda mitamboni, maafisa wakuu wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori Kenya (KWS) katika eneo la Kati hawakuwa wametoa taarifa yoyote.