Habari za Kitaifa

Sitakubali mahakama itoe maamuzi ya kukwamisha miradi yangu, Ruto aapa

January 2nd, 2024 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

Rais William Ruto ameapa kwamba hatangoja idhini za mahakama ili kutekeleza ajenda yake ya kimaendeleo kwa mujibu wa manifesto ya Kenya Kwanza, akitangaza vita kwa maafisa wa idara hiyo ambao alidai hupokea hongo kutoa ilani za kumkwamisha.

Rais Ruto alitangaza hayo Jumanne, Januari 2, 2024 akiwa katika Kaunti ya Nyandarua alikohudhuria mazishi ya babake Seneta John Methu, marehemu Michael Maigo Waweru huku akichemkia maafisa wa mahakama ambao alisema kazi yao ni kusimamisha miradi kupitia ilani za mahakama.

“Mimi ninaheshimu uhuru wa mahakama. Lakini kile sitakubali na naapa kusimamisha ni utundu, ukiritimba na ufisadi wa wachache ndani ya idara hiyo kwa kuwa walio na uwezo kwa mujibu wa katiba ni wananchi wenyewe,” akasema.

Aliagiza mawaziri na makatibu katika wizara wajiandae kuanza kutekeleza miradi ambayo imepitishwa na wananchi na mabunge yao na kisha yeye kuweka sahihi ili iwe sheria.

“Mpango wa ujenzi wa nyumba, ule wa afya kwa wote…barabara ambazo zinanuia kusaidia Wakenya…enda weka pesa tuanze utekelezaji,” akasema.

Alisema kwamba ajenda yake imetekwa nyara na “mitandao ya ufisadi iliyoenea hadi mahakamani ambako kuna wachache washirika wa kuhongwa ili wakwamishe yale ya kuwafaa Wakenya kwa masilahi ya wachache”.

Hata hivyo, matamshi yake yamekemewa vikali na aliyekuwa rais wa muungano wa mawakili nchini (LSK) Bw Okong’o Omogeni aliyesuta cheche hizo za Rais Ruto huku mahakama ikitarajiwa kutoa uamuzi kuhusu uhalali wa ushuru wa ujenzi nyumba mnamo Januari 14, 2024.

Aliitaka idara ya mahakama isitishike akimkumbusha Rais kwamba yuko chini ya taasisi kadha ikiwemo mahakama na kujaribu kukaidi mfumo wa kisheria ni kupisha mtafaruku mkuu nchini.

Hata hivyo, Rais Ruto alisema kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja ambao amekuwa mamlakani, ameshuhudia siasa za kipuzi zikitandazwa ambazo alisema nia ni kuhujumu ajenda ya kimaendeleo, kukwamiza wananchi ndani ya umasikini na kuweka taifa katika msukosuko wa kujadili masuala yasiyo na maana.

Alisema kwamba mitandao ya kula pesa za Wakenya haitaki kuona mianya ambayo imekuwa ikitumia kujinufaisha ikizibwa na kuweka wananchi katika umasikini na taifa ndani ya misukosuko ndiyo mbinu yao ya kujinusuru, akiapa kwamba hayo yatafika kikomo kwa muda usio mrefu.

“Wanapinga Wakenya wasipate afya bora, makao ya heshima…barabara…kwa mujibu wa kipengee cha 43 cha katiba ya nchi ambayo Wakenya ndio waliandika…Sio Rais aliandika hiyo akilazimisha serikali kuinua viwango vya ubora wa maisha…ilihali wao wako na bima za kiafya, magari na manyumba yanayopitia kwa barabara gharama zote zikiwa ni kwa Wakenya ao hao wanahujumu,” akasema.

Akionekana mwenye hamaki kuu, Rais Ruto alisema “umefika ule wakati tukomeshe vitisho…tumenyane miereka ya kisiasa kwa mawazo lainifu ambapo tukisema kama serikali tunafanya hili, wewe unaleta mawazo mbadala ili tuimarishe utenda kazi kwa Wakenya”.

Alisema kwamba kufikia sasa “hii mitandao imetuzoea na umefika wakati wa kuagana kwaheri na liwe liwalo, huo utundu wa kuhujumu taifa kupitia matukio yasiyo ya kizalendo nitakomesha, nawapasha mapema, haikubaliki”.

[email protected]