Habari

Sossion adai msukosuko Knut unasababishwa na TSC

September 18th, 2019 1 min read

Na SAMMY WAWERU

MSUKOSUKO katika muungano wa kitaifa wa kutetea maslahi ya walimu nchini (Knut) unatoka nje, amesema Katibu Mkuu.

Katibu mkuu wa muungano huo Wilson Sossion amesema msukosuko unaoshuhudiwa unasababishwa na tume ya kuwaajiri walimu nchini (TSC) ambayo haitaki aendelee kuhudumu kama ‘jenerali’ wa walimu.

“Masaibu ya Knut hayatoki ndani ya muungano; yanatoka nje. Tunayoshuhudia yanatoka kwa TSC,” akasema Bw Sossion mnamo Jumanne.

Kulingana na mbunge huyo maalum wa chama cha Orange Democratic Movement ODM, Knut kama muungano, umekuwa wenye umoja tangu zamani na kwamba anashangazwa na ‘njama zinazosukwa’ na wale anawataja kuwa ni mahasimu wake.

Agosti 2019 baraza la kitaifa katika muungano huo (NEC) lilimbandua Sossion na kuteua Hesbon Otieno kama kaimu Katibu Mkuu.

Hata hivyo, Sossion alipata afueni baada ya korti inayoshughulikia masuala ya ajira na leba kuamuru aendelee kushikilia wadhifa wake hadi kesi aliyowasilisha mahakamani kupinga kung’atuliwa kwake isikilizwe na kuamuliwa.

Tangu achaguliwe mbunge maalum wakosoaji wake wamemtaka ajiuzulu, hatua iliyoshinikiza TSC kumuondoa katika orodha ya walimu.

Inasemekana zaidi ya walimu 4, 000 wanachama wa Knut hawajapata mshahara wa miezi kadhaa iliyopita. Sossion hata hivyo anasema wanachama hao wameshauriwa ili wapate mshahara wamfurushe kama jenerali wao.

“Nina uungwaji mkono asilimia 99.99 na walimu. Nitang’atuka mamlakani wanachama wakiamua, mwingine ateuliwe na nitampa baraka zangu,” akasema.

Katibu huyo alisema Knut ni muungano huru unaotetea masuala ya walimu na kwamba utaendelea kwa mkondo huo siku za usoni hata akistaafu. Aliyasema hayo kwenye mahojiano na runinga ya Citizen.