Habari za Kitaifa

Spika Wetang’ula ataka mchakato wa kuunda IEBC uharakishwe

Na CECIL ODONGO September 16th, 2024 2 min read

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula sasa anataka mchakato wa kuunda Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) uharakishwe na kukamilishwa.

Bw Wetang’ula ameahidi kuwa hilo ndilo suala la kwanza litakalopewa kipaumbele Bunge la Kitaifa  likirejelea vikao vyake Jumanne, Septemba 17, 2024.

IEBC kwa sasa haina makamishina wa kutosha baada ya muhula wa kudumu kwa aliyekuwa Mwenyekiti Wafula Chebukati na makamishina wawili Boya Mulu na Abdi Guliye kukamilika 2023.

Aliyekuwa naibu mwenyekiti wa IEBC Julian Cherera na makamishina Justus Nyang’aya na Francis Wanderi nao waliamua kujiuzulu baada ya kusimamishwa kazi na Rais William Ruto.

Waliondolewa mamlakani baada ya Kamati ya Sheria na Haki katika Bunge la Kitaifa kupendekeza watimuliwe kutokana na mienendo yao kuhusu uchaguzi wa 2022.

Rais alibuni jopo lililoongozwa na Jaji wa Mahakamu Kuu Aggrey Muchelule kuwachunguza. Hata hivyo, ni Irene Masit ambaye pia alisimamishwa na Rais alipambana na kufika mbele ya jopo hilo lakini bado akapoteza nafasi yake.

Bw Wetang’ula amesema kuwa kuna masuala mengi ambayo yamesalia bila kushughulikiwa kutokana na pengo ambalo limekuwepo katika IEBC.

“Hatuwezi kuchelewesha zaidi mchakato wa kubuniwa IEBC kwa sababu hilo pia linachelewesha kuamuliwa kwa mipaka mipya na maeneo ya uwakilishi ambako chaguzi ndogo zinastahili kufanyika,” akasema Bw Wetang’ula.

Alikuwa akiongea katia Kanisa Katoliki la Chebukwa, Kaunti ya Bungoma alikohudhuria ibada ya Jumapili, Septemba 15, 2024.

Bw Wetang’ula alikuwa ameandamana na madiwani wengi akiwemo Kiongozi wa Wengi katika Kaunti ya Bungoma Juma Nyongesa.

Kuna maeneo 11 ya uwakilishi nchi ambako chaguzi ndogo zinastahili kuandaliwa lakini bado hilo halijafanyika kutokana na kutokuwepo kwa makamishna wa IEBC na mwenyekiti mpya.

Mchakato wa kuteuliwa jopo la kuwapiga msasa makamishina wapya wa IEBC ulikabiliwa na vikwazo vya kisheria kutokana na kesi iliyowasilishwa kwenye Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDT) .

Kesi hiyo iliwasilishwa na chama cha NLP ikipinga hatua ya muungano wa Azimio la Umoja kwa kumpendekeza Koki Muli wa Wiper awe mwakilishi wao kwenye jopo la kuwateua makamishina wa IEBC.

NLP ilidai kuwa mwakilishi wake Augustine Muli ndiye alifaa kuchukua nafasi hiyo na siku nne zilizopita PPDT iliamua kesi hiyo na kumtunuku Augustine nafasi hiyo na kupisha sasa uteuzi wa jopo hilo.

“Nawaomba wale ambao wamekuwa wakitatiza mchakato wa kuteuliwa jopo la kuwahoji makamishina wa IEBC watathmini athari ya hatua yao na kuruhusu nchi kusonga mbele. Kama bunge tupo tayari kuhakikisha mchakato huu unakamilika,” akaongeza Bw Wetang’ula.

Katika maeneo 11 ya uwakilishi yanayohitajika kuandaliwa kwa chaguzi, matatu ni maeneobunge ya Ugunja, Banisa na Magarini huku yaliyosalia yakiwa wawakilishi wadi.

Eneobunge la Ugunja lilisalia wazi baada ya Opiyo Wandayi kuteuliwa Waziri wa Kawi naye Mbunge wa Banisa Hassan Kullow  aliaga dunia kwenye ajali ya barabarani Machi 2023.

Mbunge wa Magarini Harrison Kombe naye hakuwa na lake baada ya Mahakama ya Juu kudumisha uamuzi wa kufutilia mbali ushindi wake mnamo Mei 31, mwaka huu, 2024.