• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
16 waaga dunia ajalini msimu wa Krismasi ukianza

16 waaga dunia ajalini msimu wa Krismasi ukianza

Na WAANDISHI WETU

ZAIDI ya watu 15 waliaga dunia katika ajali tofauti za barabarani tangu Jumatatu, katika mikasa ya mauti ambayo imerejesha kumbukumbu za nyakati za msimu wa Krismasi ambazo hukumbwa na mikasa aina hiyo.

Kufuatia ajali hizo, Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Uchukuzi (NTSA) ilitahadharisha waendeshaji magari wawe waangalifu wakati huu wa msimu wa sherehe za kufunga mwaka ambapo wananchi wengi wanasafiri.

“Ajali za barabarani huongezeka wakati wa msimu wa sherehe, nyingi zikishuhudiwa katika maeneo sugu ya ajali. Ajali nyingi hutokana na makosa yanayotendwa na binadamu,” Mkurugenzi Mkuu wa NTSA, Bw Francis Meja, alisema.

Kwenye taarifa, mkurugenzi huyo alisema madereva wana jukumu kubwa la kuepusha ajali za barabarani kwa kufuata sheria za kimsingi.

Alisema tangu serikali ianze kukaza kamba kwa utekelezaji wa sheria za barabarani, madereva 210 wamepokonywa leseni zao na kutakiwa kurejelea mafunzo ya udereva.

“Tutazidisha juhudi za kufutilia mbali leseni za madereva wasiofuata sheria za barabarani,” akasema.

Jana, watu saba walifariki lori lilipogongana na matatu iliyobeba abiria 14 katika eneo la Mlango Tatu, katika Barabara Kuu ya Nakuru-Eldoret, kaunti ya Baringo.

Afisa mkuu wa trafiki eneo la Bonde la Ufa Zero Arome alithibitisha kisa hicho akisema, saba hao, wakiwemo madereva wa magari yote mawili walikufa.

Ajali hiyo ilitokea saa kadha tu baada ya nyingine ya waendesha pikipiki wawili katika kituo cha kibiashara cha Kogoya, eneo la Oyugis, kaunti ya Homa Bay ambapo wote waliaga dunia.

Vilevile, watu wengine wawili waliaga dunia usiku wa kuamkia jana, wakati gari walimokuwa wakisafiria liligonga lori karibu na kiwanda cha simiti cha Athi River.

Mkuu wa polisi eneo la Athi River Sharma Wario alisema, dereva wa gari hilo aina ya Saloon aligonga lori hilo kutoka nyuma, mita chache kutoka sehemu ya mzunguko ya Nairobi-Namanga.

Ajali hiyo iliyotokea saa tano usiku ilikuwa saa 12 tu baada ya watu wengine watano kuaga dunia katika barabara hiyo, wakati trela lilipogonga matatu iliyokuwa na abiria 14.

Watano hao walikuwa kati ya waumini 14 wa kanisa la St Mary’s Miracle, Mombasa na walikuwa wakirejea mjini humo kutoka Siaya ambapo walikuwa wamepeleka ibada wikendi.

You can share this post!

UPORAJI: Mamilionea bila jasho

Serikali yaahirisha uzinduzi wa mtaala mpya, 8-4-4 kuzidi...

adminleo