• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Akasha: Shirika lahitaji miezi 6 kwa uchunguzi

Akasha: Shirika lahitaji miezi 6 kwa uchunguzi

Na PHILIP MUYANGA

SHIRIKA linalotwaa Mali Iliyoibwa (ARA) litahitaji miezi sita kuchunguza mali ambayo inamilikiwa na familia ya mfanyabiashara tajiri Baktash Akasha anayekabiliwa na kesi ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Afisa wa uchunguzi wa ARA Isaac Nakitare alieleza mahakama kwamba pia wanachunguza mali ya familia hiyo iliyoko katika mataifa ya Marekani na Pakistan kubaini kama ilipatikana kutokana na pesa za ulanguzi wa dawa za kulevya.

“Uchunguzi tunaofanya unahusisha mambo mengi na pia nchi mbalimbali,” akasema Bw Nakitare alipofika mahakamani kueleza sababu zilizochangia uchunguzi kwenye kesi hiyo kuchukua muda mwingi.

Afisa huyo alikuwa akitoa ushahidi wakati wa kusikizwa kwa kesi ambapo mke na mama wa mfanyabiashara huyo walitaka kuachiliwa kwa baadhi ya mali yao iliyotwaliwa kwenye kisa cha uvamizi nyumbani kwao Novemba 2014.

Uvamizi

Hata hivyo, Bw Nakitare alisema kwamba hakupewa mali yoyote ya familia ya Bw Akasha wala hakutembelea au kuhusika na uvamizi huo.

“Bado hatujaandaa notisi ya kutwaa mali yoyote kwa sababu uchunguzi unaendelea kufahamu jinsi familia hiyo ilipata mali hiyo,” akaongeza Bw Nakitare. Pia alieleza mahakama kwamba wanaendelea kuchunguza akaunti za benki zinazoshikiliwa na familia ya mfanyabiashara huyo.

Mkuu wa Kitengo cha kupambana na ulanguzi wa mihadarati Hamisi Massa naye alieleza mahakama kwamba kabla ya Baktash na nduguye Ibrahim Akasha kuhukumiwa Marekani kutokana na ulanguzi wa dawa za kulevya, walikuwa wameanza kuchunguza jinsi walivyopata mali yao.

Hata hivyo, mkewe Najma Juma na mama mkwe Fatma Akasha wanataka korti iamuru mali yao iachiliwe kwa kuwa inakiuka katiba na haki zao za kibinafsi.

Kati ya mali hiyo ni magari mawili ya kifahari, simu, bastola, mikufu ya dhahabu, herini na bangili. Familia hiyo inadai kwamba mali hiyo haihusiani na kesi ambayo ilichangia kuhukumiwa kwa mfanyabiashara huyo na nduguye wala haikununuliwa na pesa za dawa za kulevya.

Bw Baktash na nduguye Ibrahim walifungwa miaka 25 na 23 mtawalia baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki ulanguzi wa dawa za kulevya. Katika kesi hiyo walimshtaki Inspekta jenerali wa polisi, Afisi ya DPP, DCI, Kamanda wa polisi wa Pwani na Afisa wa uchunguzi wa uhalifu katika eneo hilo.

Walidai kwamba mnamo usiku wa Novemba 9, 2014 polisi walivamia makazi yao katika mtaa wa Nyali na kuanza kupekua nyumba yao kisha kuchukua baadhi ya mali yao. Walisema uvamizi huo ulilenga kuwanyanyasa ilhali waliwaruhusu makachero hao kufanya kazi yao bila pingamizi lolote.

Aidha walieleza korti kwamba wamekuwa wakipigania mali hiyo iachiliwe lakini maafisa wa uchunguzi wamekuwa wakisisitiza kwamba ilipatikana kwa njia haramu na ni sehemu ya kesi inayoendelea.

Kesi hiyo itasikilizwa mnamo Mei 5.

You can share this post!

Serikali yabuni njama kuunda maeneo mapya

Marais 10 kuhudhuria ibada ya kumuaga Magufuli Dodoma leo