• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Baraka za Joho kwa Nassir zinaashiria nini?

Baraka za Joho kwa Nassir zinaashiria nini?

UAMUZI wa gavana Hassan Ali Joho kumuunga mkono Bw Abdulswamad Nassir kumrithi kama gavana wa Mombasa unaonekana kutoa hisia tofauti tofauti ambazo zinaweza kubadilisha mwelekeo wa kampeni za kiti hicho na hususan zile za kusaka tikiti ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

Kwa sasa tikiti hiyo ya ODM inawaniwa na mfanyibiashara Suleiman Shahbal ambaye alijiunga na chama cha ODM miezi kadhaa iliyopita na naibu gavana wa Mombasa William Kingi.

Tangu Bw Joho kusema anamuunga mkono Bw Nassir, Bw Shahbal na Kingi hawajatamka lolote kuhusiana na uamuzi huo ambao unaonekana kumweka Bw Nassir katika nafasi bora ya kutwaa tikiti ya ODM.

Kulingana na wadadisi wa kisiasa, uamuzi wa Bw Joho una uzito mkubwa kwa kuwa yeye ni naibu kiongozi wa chama cha ODM.

Ingawa ilichukuwa muda mrefu kabla ya Bw Joho kusema kuwa anamuunga mkono Bw Nassir ambaye ni mbunge wa Mvita,dalili zilikuwa zimejitokeza kwani wanasiasa wanaohusishwa kwa ukaribu sana na gavana huyo wa Mombasa walikuwa washaanza kumpigia debe Bw Nassir.

Pigia debe Nassir

Mbuge wa Likoni Mishi Mboko, Seneta wa Mombasa Mohamed Faki, Mwakilishi wa wanawake Asha Mohamed na mbunge wa Jomvu Badi Twalib ambao ni baadhi ya wandani wa kisiasa wa gavana Joho waliamua kumpigia debe Bw Nassir kuchukua kiti cha ugavana wa Mombasa.

Hata ingawa Bi Mboko alikanusha vikali dhana ya kuwa wanasukumwa na Bw Joho kumuunga mkono Bw Nassir kuwania kiti cha ugavana,uamuzi wa gavana huyo hivi majuzi uliashiria picha tofauti.

“Mimi sijasukumwa na Bw Joho kumuunga mkono Bw Nassir, namuunga mkono kwa kuwa ni kiongozi anayestahili kuongoza Mombasa,”Bi Mboko aliambia Jamvi La Siasa.

Bi Mboko alisema kuwa Bw Nassir ni mwezake katika bunge la kitaifa na kwamba amefahamu siasa zake kwa muda mrefu ndiposa alionelea ya kuwa ni kiongozi bora anayefaa kuchaguliwa kama gavana wa kaunti ya Mombasa.

Mbunge huyo wa Likoni alisema kuwa anamuunga mkono Bw Nassir kwa kuwa yeye ni kiongozi ambaye anasikiza watu.

“Bw Nassir akichaguliwa nitakuwa huru kumfikia na kwamba tutajadiliana kuhusu maswala yanayowakabili watu wa Mombasa, kiongozi ni vitendo,” alisema Bi Mboko.

Hapo awali Bw Shahbal aliwapuuzilia mbali wanasiasa hao wa ODM wanaomuunga mkono Bw Nassir.

Akizungumza katika mojawapo ya mikutano yake ya kisiasa katika eneo la Old Town alisema kuwa iwapo alipambana na Bw Joho hapo awali kuwania ugavana wa Mombasa ‘acha hao wengine waje sasa’.

Bw Shahbal alisema kuwa mwaka wa 2013 aliposimama ugavana alikuwa hajui siasa na kwamba 2017 alisimama na chama ambacho watu walikuwa hawakitaki na kwamba hapo mwakani atachukuwa kiti.

“Mimi nasimama si kwa sababu nataka kuitwa His Excellency ama natafuta biashara, hiyo biashara Mungu alinipatia nashukuru,sina tamaa tena nasimama kwa sababu naamini kuwa huu mji wetu tunaweza kuubadilisha,” alisema Bw Shahbal.

Mkono wa ODM

Mchanganuzi wa siasa Prof Halimu Shauri alisema kuwa mkono wa ODM kwa matamshi ya Bw Joho ya kumuunga mkono Bw Nassir hauwezi kupuuziliwa mbali.

“Bw Joho ni mfadhili mkubwa wa chama cha ODM, kwa mwelekeo mkubwa kuna mkono wa chama katika uamuzi wa gavana huyo wa kumuunga mkono Bw Nassir,” alisema Prof Shauri.

Alisema kuwa uamuzi wa Bw Joho unamweka Bw Nassir katika kiwango cha juu tofauti na wagombaniaji wengine wa tikiti ya ODM kwa kuwa wafuasi wa Joho watamuunga mkono.

Prof Shauri alisema kuwa kwa sasa inaonekana ya kuwa asilimia kubwa ya chama cha ODM inamuunga mkono Bw Nassir.Hata hivyo aliongeza kusema kuwa kama chama ni cha kidemokrasia basi uchaguzi wa mchujo utekelezwe.

Alisema kuwa,kwa wawaniaji wengine wa tikiti ya ODM,haitakuwa rahisi kugombania tikiti hiyo ilhali Bw Nassir ashaungwa mkono na Bw Joho ambaye ni naibu kiongozi wa chama.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, katika maswala ya maendeleo Bw Joho hajakuwa na chochote cha kujivunia ikilinganishwa na wenzake wa kaunti zingine kwani miradi mingi iliyo Mombasa ni ya serikali ya kitaifa na itakuwa vigumu kwa Bw Nassir kubadili dhana hiyo.

“Bw Joho anaonekana sana kwa mambo ya kufurahisha watu kama vile kuleta wanamuziki na sio kwa maendeleo,” alisema Prof Shauri ambaye ni mkufunzi wa chuo kikuu cha Pwani,Kilifi.

Aliongeza kusema kuwa changamoto nyingine itakayomkumba Bw Nassir kwa kuonekana kuungwa mkono ni kuwa ataonekana kuwa mradi wa Bw Joho swala ambalo litakuwa ngumu kulitoa kwa wale ambao hawamuungi mkono gavana huyo wa Mombasa.

Mshauri wa kisiasa Bw Bozo Jenje alisema kuwa kuungwa mkono kwa Bw Nassir na gavana wa Mombasa kunaashiria ya kuwa chama cha ODM kina imani naye.

Bw Jenje alisema kuwa kwa kumuunga mkono Bw Nassir, basi gavana Joho anaonekana kuwa yuko tayari kutumia hata raslimali zake katika kampeni ya tikiti ya ODM na kiti cha ugavana ili Bw Nassir afaulu.

Hata hivyo Bw Jenje aliongeza kusema kuwa, kuungwa mkono kwa Bw Nassir kunaweza kuwa chanzo chake cha kukosa tikiti ya ODM au ugavana kwa kuwa watu wanaweza kumdhania kuwa mradi wa Bw Joho.

“Iwapo kutakuwa na njia ya kuonyesha kuwa hajawekwa kama mradi wa Joho itakuwa bora kwake,lakini bila hivyo haitaenda vizuri na na baadhi ya watu ndiposa inafaa ajionyeshe kama mtu ambaye anajitengemea mwenyewe,”alisema Bw Jenje.

  • Tags

You can share this post!

Raia wa Congo kulala ndani kwa siku saba

Mijeledi ya John Michuki ilivyolainisha sekta ya matatu

T L