• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
Barclays sasa yaitwa Absa

Barclays sasa yaitwa Absa

Na PETER MBURU

BENKI ya Barclays jana iliandaa hafla rasmi ya kuidhinisha ubadilishaji jina kuwa Absa, jina ambalo sasa litakuwa likitumika katika shughuli zake zote.

Wakuu wa benki hiyo walikuwa katika Makao Makuu ya Soko la Hisa Nairobi (NSE), ambapo walitangaza kuwa kufuatia ubadilishaji huo wa jina, benki hiyo inalenga kutoa huduma zaidi zitakazowanufaisha Wakenya wa chini, hasa wafanya biashara wadogo.

Ilibadili jina baada ya kuwa nchini kwa takriban miaka 104, tangu ilipofika na kuanza biashara Mombasa mnamo 1916. Benki hiyo ilikamilisha utaratibu wa kisheria wa kubadili jina Jumatatu, ambapo iliwataka Wakenya kuwa makini wasihadaiwe na walaghai wakapeana habari zao za siri.

“Tumezungumza na Wakenya ili kusikia wanachotaka. Tunatambua kuwa sekta ya chini Juakali ni ya maana sana kwa biashara nyingi ndogo nchini ndiposa tumeanzisha apu ya simu itakayotoa huduma mbalimbali,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Absa tawi la Kenya, Bw Jeremy Awori.

Alisema ubadilishaji huo wa jina pia unaifanya benki hiyo kupanua utoaji huduma kwa wateja wake, kutoka zile za kuweka na kutoa pesa pekee, hadi nyingine zaidi kama kuendesha biashara.

Hata hivyo, Absa ni jina linalotumika katika bara Afrika, na hatua ya kubadili jina ilifikiwa baada ya tawi kubwa la Barclays London, Uingereza kuuza hisa zake za soko la humu barani, likisalia kushughulika na soko la bara Uropa.

Miaka mitatu iliyopita, benki ya Barclays huko Uingereza iliuza hisa zake nyingi kwa kampuni kutoka Afrika Kusini ya Absa.

Absa iko katika mataifa 11 Afrika na imekuwa moja kati ya kampuni zenye sifa katika sekta ya benki nchini.

You can share this post!

Echesa achunguzwe alivyoingia kwa ofisi yangu – Ruto

Kalonzo sasa ataka Mombasa iwe bandari huru

adminleo