• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Bunge halina usemi kuhusu ‘Punguza Mizigo’ – Aukot

Bunge halina usemi kuhusu ‘Punguza Mizigo’ – Aukot

NDUNGU GACHANE na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa chama cha Thirdway Alliance, Dkt Ekuru Aukot, amepuuzilia mbali madai ya baadhi ya wabunge wanaopinga Mswada wa Punguza Mizigo, akisema Bunge la Kitaifa halitakuwa na usemi katika kupitishwa kwa mswada huo.

Badala yake, alisema baada ya kupitishwa na mabunge 24, utapita kwenye kura ya maoni.

Kulingana naye, mswada huo utawasilishwa kwa Wakenya kuupigia kura na jukumu la Bunge litakuwa tu kujadili uzuri ama ubaya wa mapendekezo yake.

Mswada huo unalenga kupunguza idadi ya wabunge kutoka 416 hadi 147, na kuongeza mgao wa fedha za kaunti hadi asilimia 35.

Akihutubu jana katika Kaunti ya Murang’a, baada ya kukutana na madiwani, Dkt Aukot alisema mapendekezo yao yanalenga kuwapunguzia mzigo Wakenya na kuupa nguvu mfumo wa ugatuzi ili kustawisha uchumi.

“Ikiwa tutapata uungwaji mkono wa angaa kaunti 24, tutakuwa tumepita kigezo cha kuandaliwa kwa kura ya maoni. Bunge la Kitaifa litapewa tu nafasi ya kujadili mapendekezo yake,” akasema.

Aliwaomba madiwani kupitisha mswada huo, akisema kuwa utawapunguzia Wakenya gharama ya juu kuendesha Bunge kutoka Sh36.8 bilioni hadi Sh5 bilioni kwa mwaka. Alisema kuwa hilo litawaokolea Wakenya Sh31.8 bilioni.

Licha ya hayo, mswada huo ulikosolewa na baadhi ya madiwani, wakisema kuwa kuna vipengele vingi vinavyohitaji ufafanuzi zaidi.

Wakati huo huo, Baraza la Maspika wa Kaunti (CAF) limesema kuwa litatoa msimamo huru kuhusu Mswada wa Punguza Mizigo, bila kuzingatia yale yatakayotolewa na vyama vyao kuhusu mswada huo.

Mwenyekiti wa baraza hilo Bw Ndegwa Wahome, alisema kwamba, wanashauriana na mawakili wao wa kikatiba, ili kuhakikisha msimamo watakaotangaza utazingatia matakwa ya wananchi.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, baraza hilo lilisema kuwa, lengo lake ni kuhakikisha kuwa msimamo litakaotoa utalingana na maoni ya wananchi wengi.

“Hatutashawishiwa na yeyote kutoa msimamo wetu. Ikumbukwe kuwa mabunge ya kaunti ndiyo yatakuwa na usemi mkuu kwenye maamuzi ya mswada huo. Tunashauriana na wadau mbalimbali kabla ya kutangaza rasmi msimamo wetu,” akasema Bw Wahome.

Tayari, vyama vya ODM na Wiper vimetoa misimamo yao rasmi kuhusu mswada huo. Wiki iliyopita, ODM, ilikosoa mswada huo, ikisema haujatoa utaratibu wa ushirikishi katika Serikali Kuu na njia itakayotumiwa kukabili deni la kitaifa ambalo linazidi kuongezeka.

Kwa upande wake, Wiper ilikosoa chama cha Thirdway Alliance, ikisema hakikuushirikisha umma katika uandaaji wa mswada huo.

Hata hivyo, walisema kwamba wanaunga mkono pendekezo la kuongezwa kwa mgao wa fedha za kaunti kutoka kwa serikali ya kitaifa, kwani ni baadhi ya mambo ambayo wamekuwa wakipigania.

“Ingawa hatujatoa msimamo rasmi, utathmini wetu wa mwanzo mwanzo kuhusu mswada huu ni kwamba, unaashiria hatua nzuri kwa masuala ambayo tumekuwa tukiyapigania kama Wakenya. Tutayashirikisha mabunge yote 47 ili kuutathmini kwa undani,” akasema Bw Wahome.

You can share this post!

Familia ya Ken Okoth yalia kutohusishwa kwa mipango ya...

Gavana kikaangoni kutumia fedha zaidi kulipa mishahara

adminleo