• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Capwell yaendelea kujizolea umaarufu Ligi ya Kanda ya Kati

Capwell yaendelea kujizolea umaarufu Ligi ya Kanda ya Kati

Na LAWRENCE ONGARO

INGAWA ilibuniwa miaka miwili iliyopita, Capwell ni timu ambayo imepiga hatua kubwa hasa kwa kuingia Ligi ya Kanda ya Kati Zoni A.

Kocha wake Haji Bilali anasema licha ya kupitia changamoto tele, wanajivunia kufikia kiwango hicho.

Mwaka wa 2021 timu hiyo ilishiriki Ligi ya kaunti ndogo ya Thika na kumaliza katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 43.

Kwa wakati huu timu hiyo inashiriki Ligi ya Kanda ya Kati ambapo imezoa pointi 12 baada ya kucheza mechi 11.

Timu hiyo imeshinda mechi tatu na kutoka sare mechi tatu huku ikipoteza mechi tano.

Hata hivyo kocha anasema baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo hivi majuzi, anatarajia kuleta mabadiliko machache kikosini ili kuleta uhai mpya kwenye timu.

Baadhi ya wachezaji wake wanaoletea kikosi sifa tele ni Shem Karanja ambaye ni kipa, Mathew Mwema, Lawrence Otieno, Elisha Otieno na Isaac Kimani. Pia kuna Benjamin Kipsang ambaye ni nahodha wa timu, David Kamau na Brian Mureithi. Halafu kuna Lawrence Ogambo, Mathew Macharia na Lokatuken Titaus.

Kocha Bilali anasema ana mpango wa kukuza talanta za vijana wa timu hii kupitia mazoezi kabambe.

Anasema nia yake kuu ni kumaliza ligi katika nafasi ya tano-bora huku akiamini azma yake itatimia.

Anataja timu kama Ganaki, Blue Nile, Gathanga na Maisha Mabati kama baadhi ya klabu zinazoleta ushindani mkubwa katika ligi hiyo.

Anaeleza kuwa kwa wakati huu anajivunia kuwa na wachezaji 28 ambao wamesema watacheza kwa bidii.

Anampongeza meneja wa timu ambaye ni Edwin Githondu ambaye ameonyesha kuwa ana nia njema ya kuisukuma timu hiyo katika kiwango kingine cha juu.

Anataja nidhamu na kujiamini kama chanzo cha kikosi chake kujizatiti katika ligi hiyo.

Anasema mazoezi huwa ni kila siku ya Jumanne hadi Ijumaa ili kukipa kikosi nguvu ya kupiga hatua.

Anaeleza kuwa mchezaji yeyote ambaye hahudhurii mazoezi huwa hapati nafasi ya kucheza mechi, na kwa hivyo kila mmoja lazima afuate sheria hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Wa Iria asisitiza yuko katika kinyang’anyiro cha urais

MAKALA MAALUM: Jinsi Ruto anavyopanga kuuzima umaarufu wa...

T L