• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 10:55 AM
Chuo Kikuu cha Auburn kumfaa nyota Angella Okutoyi kujiendeleza

Chuo Kikuu cha Auburn kumfaa nyota Angella Okutoyi kujiendeleza

Na GEOFFREY ANENE

MWANATENISI Angella Okutoyi hatimaye ametangaza chuo kikuu atakachoendeleza tenisi yake na masomo.

Kupitia mitandao ya kijamii, bingwa huyo wa tenisi ya chipukizi ya wachezaji wawili kila upande ya Wimbledon amesema kuwa atajiunga na Chuo Kikuu cha Auburn katika jimbo la Alabama, Amerika.

“Nafurahi sana kutangaza kuwa nitaendeleza taaluma yangu ya tenisi na masomo katika Chuo Kikuu cha Auburn! Shukran ziendee familia yangu, makocha, marafiki na kila mtu aliyenisaidia kufika hapa!” alisema mwanafunzi huyo wa zamani wa shule ya msingi ya Loreto Convent na Mbagathi jijini Nairobi na kituo cha Shirikisho la Kimataifa la Tenisi (ITF) nchini Burundi.

Okutoyi, 18, ataelekea Amerika mwezi Januari 2023 baada ya kushiriki mashindano mawili ya wanawake ya tuzo ya Dola 15,000 za Amerika (Sh1.8 milioni) ya W15 Monastir nchini Tunisia mnamo Oktoba 17-23 na W15 Nairobi uwajani Karen Country Club jijini Nairobi mnamo Novemba 14-20.

Bingwa huyo wa Kenya Open 2018 na Afrika kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 18 mwaka 2021 aliandikisha historia mwaka huu kwa kushiriki mashindano yote manne ya haiba ya Grand Slam ya chipukizi nchini Australia, Ufaransa, Uingereza na Amerika.

Alishinda Wimbledon katika kitengo cha wachezaji wawili kila upande akishirikiana na Mholanzi Rose Marie Nijkamp mwezi Julai.

Okutoyi anayeshikilia nafasi ya 52 kwenye viwango bora vya chipukizi vya ITF vya Oktoba 10, aliitiwa udhamini wa masomo kutoka zaidi ya vyuo vikuu 30 nchini Amerika kabla ya mashindano ya US Open.

Alitembelea vyuo vikuu vya Auburn, California Berkeley, Central Florida na North Carolina State kabla ya kuamua Auburn itamfaa zaidi. Akiwa Auburn pia atasomea digrii ya Usimamizi wa Biashara.

  • Tags

You can share this post!

Cristiano Ronaldo afikisha mabao 700 tangu aanze kusakata...

Kero ya taka katika daraja la Kayaba-Hazina

T L