• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Covid-19: 133 zaidi waambukizwa

Covid-19: 133 zaidi waambukizwa

Na CHARLES WASONGA

KENYA imeandikisha visa 133 vya Covid-19 Jumatatu hivyo kufikisha 3,727 idadi jumla ya maambukizi ya ugonjwa huo nchini.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema visa hivyo vipya vilipatikana baada ya sampuli 3,365 kufanyiwa uchunguzi ndani ya muda wa saa 24 tangu Jumapili.

Vile vile aliyangaza kuwa jumla ya wagonjwa 33 wamepona na kuruhusiwa kwenda nyumbani huku mmoja akifariki.

“Kwa hivyo, kufikia leo (Jumatatu) jumla ya 1,286 wamepona huku jumla ya watu 104 wakifariki,” akawaambia wanahabari katika katika Hospitali ya J.M Kariuki mjini Olkalou, Nyandarua.

Kufikia Jumatatu jumla ya sampuli 180,701 zilikuwa zimepimwa.

Visa 133 vipya vya maambukizi ya virusi vya corona vimesambaa katika kaunti zifuatazo; Mombasa (61), Nairobi (53), Kilifi (7), Busia (6), Kiambu (2) huku Kajiado, Murang’a, Nakuru na Kitui zikiandikisha kisa kimoja kila moja.

Katika kaunti ya Nairobi kati ya visa 53, eneo bunge la Mathare limeandikisha visa 10, Kamukunji (9), Westlands (6), Starehe (5), Makadara (4) huku Embakasi Magharini, Embakasi Mashariki na Kibra kila moja yakiwa na visa 3 kila moja.

Maeneo bunge Ruaraka, Embakasi Kusini na Kasarani yameandikisha visa viwili kila moja huku Embakasi ya Kati, Dagoretti Kaskazini, Dagoreti Kusini na Langata yakiwa ni kisa kimoja kila moja.

Katika kaunti ya Mombasa, visa 61 vilipatikana Likoni, Mvita (19), Nyali (7), Kisauni (5), Changamwe (5) na Jomvu (1).

Wakati wa ziara yake ya kukagua hospitali mbalimbali katika kaunti ya Nyandarua, Waziri Kagwe aliipongeza kuwa kutoandikisha kisa chochote cha Covid-19.

“Nashauri raia wote kuendelea kuzingatia masharti yaliyowekwa na serikali ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona kama vile kuvalia barakoa. Kama ambavyo nimekuwa nikisema kila mara, wajibu wa kudhibiti ugonjwa huu ni wa kila mtu,” Bw Kagwe akasema.

You can share this post!

Mahakama zaanza kushughulikia kesi

Nyandarua yasifiwa kutilia maanani kanuni za Covid-19

adminleo