• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Dhuluma za kimapenzi dhidi ya wanawake zachacha Sudan Kusini

Dhuluma za kimapenzi dhidi ya wanawake zachacha Sudan Kusini

CHARLES WASONGA Na MASHIRIKA

JUBA, Sudan Kusini

MAMIA ya akina mama na wasichana wamekuwa wakinajisiwa na kutendewa aina zingine za unyama kwa muda wa siku kumi zilizopita kaskazini mwa Sudan Kusini, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limesema.

Mhudumu mmoja wa afya katika shirika hilo alisema katika muda wa siku 10 zilizopita jumla ya wanawake 125 walifika katika kliniki yao iliyoko eneo la Bentius kusaka huduma ya matibabu baada ya kudhulumiwa.

Idadi hiyo ni juu zaidi kuliko ile ambayo imeshuhudiwa katika muda wa miezi 10 iliyopita.

“Miongoni mwao ni wasichana wenye umri wa chini ya miaka 10, wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 65 na wengine ambao wajawazito,” akaongeza mhudumu huyo ambaye hakutaka kutambuliwa kwa jina.

Taifa hilo limekuwa likizongwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu lilipata uhuru wa kujitawala kutoka Sudan mnamo mwaka wa 2011. Hata hivyo, mapigano yalizuka baada ya miaka miwili huku eneo la Bentiu likiwa moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi.

Mkataba wa amani ulitiwa saini mwezi Septemba mwaka huu kati ya mrengo wa serikali na ukiongozwa na Rais Salva Kiir na ule wa kiongozi wa waasi Riek Machar.

Mhudumu mwingine wa afya kwa jina Ruth Okello pia alithibitisha kuwa idadi ya visa vya dhuluma za kimapenzi iliyoripotiwa katika kliniki ya iliyoko Bentiu, jimboni Unity, imeongezeka zaidi katika siku chache zilizopita.

“Kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu ambao nimekuwa nikifanyakazi kazi Sudan Kusini, sijawahi kushuhudia ongezeko la waathiriwa wa dhuluma za kimapenzi kiwango hiki wakisaka hudumu za afya katika kliniki yetu,” akasema.

You can share this post!

Shule zafungwa Ivory Coast baada ya askari jela kulimana na...

FUNGUKA: ‘Tunavyosisimua ladha chumbani…’

adminleo