• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Equity Bank FC mabingwa taji la mashirika ya kifedha

Equity Bank FC mabingwa taji la mashirika ya kifedha

Na JOHN KIMWERE

TIMU mbili za Equity Bank FC zilionyesha ubabe wazo katika soka na kutawazwa wafalme na malkia kwenye michezo ya taji la Mashirika ya Kifedha nchini (Interbanks) 2019 iliyofanyika uwanja wa KSMS, Nairobi.

Timu ya wanaume ya kocha, Zuberi Mohamed ilihifadhi taji hilo ilipobugiza KCB magoli 4-1 katika fainali.

Equity ilitandaza soka safi na kusajili ufanisi huo kupitia Abshiri Abubakar magoli mawili, nao Brian Kipkemboi na David Wahome kila mmoja aliitingia goli moja.

Goli la kufutia machozi la KCB ya kocha, Lamech Ogum lilifunikwa kimiani na Samuel Mrisho. Nayo Bank of Afrika (BOA) ilimaliza ya tatu baada ya kuranda ECO Bank FC bao 1-0.

Wachezaji wa kikosi cha Gulf African Bank waliobanduliwa katika robo fainali za michezo ya Mashirika ya Kifedha nchini (Interbanks) kwa kulazwa mabao 2-0 na ECO Bank. Picha/ John Kimwere

Kitengo cha kina dada, Equity Bank ilikusanya alama kumi na kuibuka mabingwa wa mwaka huu. Equity iliandikisha ufanisi wa mechi tatu kwa bao 1-0 kila moja dhidi ya KCB, Co-operative Bank na I & M, kisha iliagana sare tasa na Barclays Bank of Kenya (BBK) kabla ya kukubali kulala kwa bao 1-0 mbele ya Central Bank of Kenya (CBK).

”Sina shaka kupongeza timu zote mbili kwa kuonyesha mchezo safi na kubeba taji la mwaka huu ambapo haikuwa rahisi hasa kitengo cha wanaume kuhifadhi ubingwa huo,” alisema meneja wa Equity, Ben Juma.

Kwenye nusu fainali Equity Bank iliangusha BOA kwa mabao 2-0 huku ECO Bank ikinyukwa magoli 3-1 na KCB.

Kwenye mechi za robo fainali, Equity Bank iliyoibuka kati ya vikosi vilivyoteremsha soka ya kupendeza kuanzia mwanzo wa kipute hicho ilitwaa ufanisi wa mabao 2-1 dhidi ya National Bank of Kenya (NBK), KCB ilipata ushindi sawa na huo mbele ya Consolidated Bank FC, Gulf African Bank FC (GAB) ililimwa mabao 2-0 na ECO Bank huku Bank of Afrika (BOA) ikilaza Central Bank of Kenya (CBK) mabao 2-1.

Mchezaji wa Equity Bank FC, Daniel Muthendu (wa pili kulia) akishindana na wachezaji wa Kirigiti Community FC. Equity ilihifadhi taji la Michezo ya Mashirika ya Kifedha nchini (Interbanks) baada ya kulaza KCB mabao 4-1. Picha/ John Kimwere

Kwenye michuano ya mchujo, Equity Bank iliyokuwa imepangwa Kundi A iliibuka kileleni kwa alama 13, mbili mbele ya KCB.

Kundi B, BOA ilimaliza ya kwanza kwa alama 15, nne mbele ya GAB. Nazo Consolidated Bank FC na ECO Bank kila moja ilimaliza nafasi ya kwanza kwa alama 14 na nane kwenye jedwali ya Kundi C na D mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

Oserian Ladies watiwa adabu tena na Zetech Sparks

Malkia Strikers wajifariji kwa kupiga Cameroon

adminleo