• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Havi akaa ngumu

Havi akaa ngumu

Na BENSON MATHEKA

MWENYEKITI wa Chama Cha Wanasheria nchini (LSK), Nelson Havi amepuuza hatua ya wanachama wa baraza la chama hicho kumsimamisha kazi akisema hawana uwezo wa kumuondoa ofisini.

Mnamo Jumatatu, baadhi ya wanachama wa baraza la LSK walimsimamisha kutekeleza majukumu yake likisema hana uwezo wa kuongoza chama.

“Tunamsimamisha Nelson Andayi Havi kutoka ofisini na kutekeleza majukumu ya mwenyekiti wa Chama Cha Wanasheria nchini kuanza Februari 8 2021 hadi Machi 27 2021 wakati mkutano wa kila mwaka utaandaliwa na ajitee binafsi au kupitia wakili wake na baadaye uamuzi utafanywa katika mkutano huo kupitia kura ya wanachama wote watakaohudhuria,” baraza lilisema kwenye taarifa.

Lakini Bw Havi alisema kwamba hawezi kuondolewa ofisini na baraza la wanachama wanane pekee akisema mwenyekiti anaweza kuondolewa kupitia mkutano wa wanachama wote wa LSK.

Alisema kwamba waliodai kwamba wamemsimamisha walisimamishwa kutoka baraza la chama hicho

“Wanachama wanane wa baraza waliosimamishwa hawana nguvu za kumsimamisha mwenyekiti wao Nelson Havi. Hilo ni jukumu la wanachama katika mkutano mkuu,” alisema na kuapa kwamba ataendelea kuhudumu hadi kipindi chake kitakapokamilika Machi 24, 2022.

Bw Havi alidai kwamba waliomsimamisha wanataka kuiba pesa za chama.

Mnamo Januari 18, 2021, wanachama wa baraza la LSK Bernhard Ng’etich, Ndinda Kinyili, Faith Odhiambo, Riziki Emukule, Aluso Ingati, Beth Michoma, Carolyne Mutheu na George Omwansa walisimamishwa kwenye mkutano wa wanachama.

Hata hivyo, walienda kortini na hatua hiyo ikabatilishwa. Mnamo Jumatatu waliungana kumsimamishwa Bw Havi huku wakijiandaa kuwasilisha mswada wa kumuondoa ofisini kwenye mkutano wa mwaka wa wanachama wote mwezi ujao.

  • Tags

You can share this post!

BI TAIFA FEBRUARI 9, 2021

Fahali anayeenda haja chooni kama binadamu azua hofu kwa...