• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Hoteli iliyovamiwa na magaidi yauzwa

Hoteli iliyovamiwa na magaidi yauzwa

Na BRIAN OCHARO

MMILIKI wa Hoteli ya Paradise Beach ambayo ilishambuliwa kwa bomu na magaidi wanaohusishwa na Al Qaeda mwaka wa 2002, ameamua kuiuza kutokana na hasara.

Stakabadhi zilizoonwa na Taifa Leo zinaonyesha kuwa hoteli hiyo iliyokuwa ya kifahari inauzwa kwa Sh800 milioni baada ya kupoteza biashara kwa miaka 21 kutokana na uvamizi huo.Hoteli hiyo imejengwa katika ardhi ya ekari 20 eneo la Kikambala, Kaunti ya Kilifi, mita 100 kutoka Bahari ya Hindi.

Hoteli hiyo yenye vitanda 340 ilianza kupata hasara baada ya shambulio la kigaidi lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 13.Katika mahojiano ya awali na Taifa Leo, msamimzi wa hoteli hiyo, Bw Yehuda Sulami alisema hoteli hiyo ilianza kupoteza biashara baada ya kuvamiwa na magaidi.

Bw Sulami ambaye pia ni mwenyekiti wa kampuni ya Simba Group Kenya alisema bomu hilo lilivuruga biashara katika hoteli hiyo ambayo ilitegemea watalii kutoka Israeli, Ujerumani, Ufaransa, Italia na nchi nyingine za Ulaya.’Jitihada za kufufua hoteli hii hazijazaa matunda. Hatuna budi ila tumelazimika kuiuza,’ alisema.

Kwa miaka mingi, usimamizi wa hoteli hiyo umejaribu kufufua biashara hiyo kwa kushawishi watalii wa ndani lakini juhudi hizo hazijafaulu.Kulingana na Bw Sulami, Wazungu waliacha kumiminika katika hoteli hiyo kwa kuhofia kulengwa na magaidi.

Shambulio hilo la kigaidi lilisababisha ndege za kukodisha kutoka Uropa, ambazo zilikuwa zikileta hadi wageni 270 kwa kila ndege, kupunguza kabla ya kusimamisha huduma huku hoteli hiyo ikibaki ikihangaika kutafuta watalii wa ndani.Katika jaribio la kurudisha umaridadi wake, zaidi ya Sh300m zimetumika kuikarabati hoteli hiyo lakini kwa sababu ya ukosefu wa wateja, imebaki mahame.

Hoteli hii ni moja ya hoteli katika eneo la Pwani ambazo zimeteseka kwa sababu ya vitisho vya ugaidi.Wakati hoteli nyingine zimenusurika vitisho na zinajitahidi kubaki katika biashara, hoteli hii inayomilikiwa na raia huyo wa Israeli imeamua kujiondoa kwenye soko la utalii la Kenya.

Shambulio hilo la kigaidi la Al Qaeda la Novemba 28, 2002 lilitokea wakati mshambuliaji wa kujitoa mhanga alipolipua hoteli hiyo na kuwaua Wakenya na wageni wakiwemo raia wa Israeli.

You can share this post!

Kipchirchir aweka rekodi mpya ya Eldoret Marathon

Tanzania kuanza zoezi la utoaji chanjo dhidi ya gonjwa la...