• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Kang’ata aandika barua akilia kuhusu kuharibika kwa mitambo spesheli ya matibabu hospitalini Murang’a

Kang’ata aandika barua akilia kuhusu kuharibika kwa mitambo spesheli ya matibabu hospitalini Murang’a

NA MWANGI MUIRURI

SERIKALI ya Kaunti ya Murang’a imetoa tahadhari ikisikitika huenda wenyeji na wakazi wakakosa kupata matibabu ya magonjwa hatari kufuatia kuharibika kwa mashine muhimu.

Kupitia ilani ya Desemba 15, 2023, iliyochapishwa katika ukurasa rasmi wa serikali hiyo katika mtandao wa Facebook, ilielezea kwamba serikali kuu ndiyo ya kulaumiwa katika hatari hiyo.

“Serikali kuu mnamo mwaka 2018 ilitoa mashine za CT scan, X-ray, MRI na nyingine kadha katika idara za upasuaji kwa hospitali za Level 5 kote nchini. Lakini aliyekuwa ameshirikiana katika mpango huo akiwa ni kampuni ya Mega Scope and General Electric-GE companies kwa sasa amejiondoa katika kukarabati mashine hizo,” taarifa hiyo ikasema.

Ilani hiyo iliongeza kwamba hali hiyo imeishia kusambaratisha huduma kwa kiwango kikuu, hali ambayo itaishia kuathiri wagonjwa wanaosaka huduma za kimatibabu katika hospitali ya Murang’a ambayo ndiyo ya kipekee ya kiwango cha Level 5.

“Sisi kama Kaunti tunanuia kukarabati mashine zile kuukuu tulizokuwa nazo huku tukingoja maelewano ya serikali kuu na kampuni hiyo iliyotoa mashine hizo kwa njia ya mkopo yatakayoishia hali hiyo kurekebishwa,” ilani hiyo ikaongeza.

Serikali hiyo ya Bw Irungu Kang’ata iliomba msamaha kwa wenyeji ikizingatia watakaoathirika wawe na subira, waelewe ni kwa nini kwa muda watakuwa wakiagizwa kusaka huduma katika hospitali mbadala hasa ile ya Kenyatta jijini Nairobi, hali ambayo itazidisha mahangaiko na gharama ya kupata matibabu kupanda.

Seneta wa Murang’a Joe Nyutu alisema kwamba “hii ni hali mbaya na ambayo haistahili hasa wakati huu tunajizatiti kuafikia afya bora yenye gharama ya chini kwa wananchi wote”.

Bw Nyutu alisema mzozo kati ya serikali kuu na kampuni iliyotoa mashine hizo unafaa kutatuliwa haraka iwezekanavyo ama serikali za Kaunti zipewe umiliki wa mitambo hiyo ili zisake afueni ya ukarabati.

“Hatuwezi kuwa taifa ambalo linatekeleza afya kwa wote na kwa mpigo tunasema hatuna mashine muhimu za kusaidia jitihada hizo. Hili ni suala nitazingatia kwa karibu sana katika serikali ya Rais William Ruto ambaye niko na uhakika hata yeye anasononeka kufuatia hali hii ya sasa,” akasema.

Bw Nyutu alisema kwamba Waziri wa Afya Susan Nakhumincha anafaa kuwa tayari ametatua suala hilo kwa kuwa ni la umuhimu sana katika kuangazia utendakazi wa serikali kwa ujumla.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Nina wawili ila kwa sasa mwenzenu niko singo, adai Samidoh

Gachagua ataka Wakenya wampe Rais Ruto muda wa kuimarisha...

T L