• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Heko Mama Samia, Dkt Ruto na Mzee Museveni kuimarisha uhusiano wa Afrika Mashariki

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Heko Mama Samia, Dkt Ruto na Mzee Museveni kuimarisha uhusiano wa Afrika Mashariki

NA WALLAH BIN WALLAH

NCHI tatu za Afrika Mashariki: Kenya, Uganda na Tanzania ni ishara ya mafiga matatu ya kuinjikia chungu mekoni.

Nchi moja ikijiondoa ama kujitenga, chungu cha Afrika Mashariki hakiinjikiki, hakitokoti, hakipwagiki wala chakula cha wana wa Afrika Mashariki hakitapikika kamwe.

Ni faraja na fahari kubwa kwetu wananchi wa Afrika Mashariki kuwaona viongozi wetu watatu Mama Samia Suluhu Hassan, Dkt William Samoei Ruto na Mzee Yoweri Kaguta Museveni wakikutana kwa furaha na bashasha kusuka masuala ya maendeleo, maisha, uhusiano wa kibiashara na mustakabali wa uchumi wa nchi zetu.

Ndugu wapenzi, uhusiano na ujirani mwema ni muhimu sana katika kuimarisha amani, upendo, maendeleo, uchumi na undugu katika nchi zinazopakana ambazo zina mkabala wa historia inayoshabihiana kidini, kijamii, kisiasa, kiuchumi, kimazingira pamoja na usuli wa kutumia lugha moja ya Kiswahili kama tulivyo Afrika Mashariki.

Majadiliano

Hatua ya Rais wa Kenya Dkt William Ruto kuzuru nchi jirani za Uganda na Tanzania kujadiliana na viongozi wenzake ili kuimarisha zaidi ujirani mwema na kukwazua vikwazo vya usafiri, uchumi na biashara mipakani ni neema kubwa kwa nchi zetu. Heko sana viongozi wetu.

Pongezi zaidi ziwafikie Mama Samia Suluhu na Dkt William Ruto kwa kutumia lugha ya Kiswahili walipozungumza kuhusu vipengele kadhaa vya miradi na uchumi wa Kenya na Tanzania. Bila shaka hadhi ya Kiswahili itaongezeka. Mungu ibariki Afrika Mashariki.

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Kinaya cha Kiswahili kuenziwa mno ughaibuni...

GWIJI WA WIKI: Carolyne Wekesa

T L