• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KEN OKOTH: 1978 hadi 2019

KEN OKOTH: 1978 hadi 2019

Na MWANGI MUIRURI

IKIWA mtu ni utu, basi wengi wa wenyeji wa eneobunge la Kibra katika Kaunti ya Nairobi wanasema kuwa marehemu mbunge wao, Ken Okoth alikuwa mtu halisi.

Okoth alikuwa Mkristo aliyeishi maisha ya kujaliana hali na kufaana kwa dhiki na pia katika faraja na Wakenya waliokuwa karibu naye.

Mchuuzi mmoja jijini Nairobi anammiminia sifa.

“Hakuwa na ubaguzi. Alikuwa mbunge wa jamii zote za hapa Kibra na ungependa kukosana naye kabisa, mwendee kwa msingi kuwa wewe ni Mjaluo ukisaka unyanyase mwingine wa jamii ya wengine,” anasema mchuuzi Milka Achieng’ ambaye shughuli zake ni za jijini Nairobi.

Sunday Ochieng’ akiwa makanga katika magari ya jijini kuelekea Kibra kupitia Hurligham anasema kifo hakibagui.

“Kimemnyakua mwanasiasa ambaye alikuwa ndiye uso wa utu na utumishi kwa wote bila ubaguzi,” anasema Ochieng’.

Hata hivyo, atakumbukwa kama mmoja wa wabunge ambao walikuwa wakipigia debe kilimo na utumizi wa bangi nchini akisema kuwa ilikuwa ni dawa na mmea wa faida.

Aliaga Ijumaa katika Nairobi Hospital ambako alikuwa amepelekwa Alhamisi kupokea matibabu akiwa katika hali mbaya kiafya ambapo alikuwa akiugua saratani ya utumbo.

Mzawa wa mwaka 1978, aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 41 na ambapo kumbukumbu zake njema ni kuwa alikuwa na weledi tosha wa usemi na wa kuenzi maendeleo.

Aliaga dunia baada ya wiki mbili za kuonekana akiwa mkakamavu hadharani licha ya ishara kuwa wazi kuwa kilichokuwa kikimwandama mwilini kilikuwa kinamla polepole.

Ni mauti ambayo yaliwaguza wengi nyoyoni hasa vijana jijini na kwa umoja wa hisia za maombolezi, wakaomba atakayerithi mikoba yake katika eneo bunge hilo awe ni mtu wa matendo, mapenzi na upana wa kiutu sawa na mwendazake.

Alikuwa amelazwa katika hospitali moja nchini Ufaransa kwa muda wa miezi mitano.

Mpenzi wa nyimbo za Kiafrika, Bw Okoth amelikunja jamvi la maisha yake wakati alihitajika kuungana na Wakenya wa nia njema kuunganisha taifa hili ambalo linapitia mkondo wa siasda za hila na njama uchaguzi mkuu wa 2022 ukiwadia.

Ni takribani kipindi cha wiki mbili tu zilizopita ambapo mbunge huyo alikuwa amerejea nyumbani kutoka Ufaransa ambako alikuwa akipokea matibabu kwa miezi mitano.

Bw Okoth alichaguliwa mara ya kwanza mwaka wa 2013 kwa tiketi ya uaminifu kwa kinara wa Upinzani, Raila Odinga na ambapo alikuwa amejishindia sifa za kuwa mmoja wa waratibu mufti zaidi wa hazina za maendeleo mashinani (NGCDF), awali ikijulikana kama CDF.

Alikuwa mmoja wa waliokuwa wakipigiwa upatu wa kuwania ugavana wa Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2022 na kupitia kwa uwekezaji wake wa imani kwa makabila yote, apae kwa urahisi.

Alizaliwa katika kijiji cha Kisumu Ndogo ndani ya mtaa wa mabanda wa Kibra mwaka wa 1978 akiwa wa nne katika familia ya watoto sita

“Babangu aliingia mitini wakati majukumu ya kulea familia yetu kubwa yalimlemea na akatuacha chini ya ulezi wa mamangu mzazi… Tulikuwa tukiishi katika kibanda cha futi 10 kwa 10 karibu na mkondo wa garimoshi na ambapo hatari kuu ya kumalizwa na treni ilikuwa ikitukodolea macho kila wakati tukiwa ndani ya kibanda hicho,” akanukuliwa akisema akiwa katika uhai wake.

Mungu wa waja alimnusuru kutoka maisha hayo ya uchochole kupitia kumpa akili pevu na ambapo alihitimu mtihani wake wa KCPE na akajiunga na Starehe Boys Centre na kisha Chuo Kikuu cha St Lawrence nchini Amerika alikofuatilia taaluma ya Mahusiano ya Kimataifa.

Alifuatilia uzamili katika kozi hiyo katika Chuo Kikuu cha Georgetown na akiondoka katika uhai wake, alikuwa amemuoa Mzungu na kujaliwa watoto.

Ni katika ushuhuda wake akiwa hai kwamba ashawahi kufanya kazi za kibarua jijini, akiwa askarirungu na pia mchuuzi wa magazeti na pia kama mpokezi wa wageni katika hospitali ya Masava jijini Nairobi.

Kabla ya kuaga dunia, alikuwa kipenzi cha wabunge wengi na ambapo alikuwa habagui ushirika wake kwa msingi wa kabila, chama au dini.

Okoth ameacha nyuma wakfu wa Okoth ambao alikuwa akiutumia kuwaokoa waja wa Kibra ili kuafikia masomo, matibabu, makazi na lishe na alijulikana kwa kupenda kusoma, kucheza soka na kujadiliana.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Mke hanipi tena joto, asema ndoa...

Watu mashuhuri walioangamizwa na kansa

adminleo