• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kihara akata rufaa kupinga uamuzi kuhusu majaji 41

Kihara akata rufaa kupinga uamuzi kuhusu majaji 41

Na RICHARD MUNGUTI

HUENDA uteuzi wa majaji 41 ulioagizwa utekelezwe na Rais Uhuru Kenyatta katika muda wa siku 14 ukacheleweshwa baada ya Mwanasheria Mkuu Paul Kihara kukata rufaa.

Bw Kihara alisema Serikali haikuridhishwa na agizo la majaji watatu Lydia Achode, Enoch Mwita na James Makau kumtaka Rais Kenyatta awateue majaji hao 41.

Katika uamuzi uliotolewa Alhamisi majaji hao walisema Rais alikosea kuchelewesha kuwateua majaji 41 walioidhinishwa na tume ya kuajiri watumishi wa idara ya mahakama JSC.

Majaji walisema kuwa “ kisheria Rais hana mamlaka ya kuhoji ama kufanyia marekebisho majina ya majaji walioteuliwa na JSC.”

Katika taarifa iliyotolewa na afisi ya mwanasheria mkuu , serikali imeeleza kutorodhika kwake na uamuzi huo na kuwasilisha arifa ya dharura katika mahakama kuu.

“Afisi ya mwanasheria mkuu imepokea nakala ya uamuzi huo wa majaji watatu na imeanza utaratibu wa kukata rufaa,” ilisema arifa hiyo yakuwasilishwa kwa rufaa.

Mwanasheria mkuu amesema kuwa hajaridhishwa na jinsi majaji hao walitafsiri sheria na itabidi atafute haki zaidi katika mahakama ya rufaa.

“Tumewasilisha arifa ifaayo katika mahakama ya rufaa pamoja na kuomba mahakama kuu itoe ushahidi wote uliotolewa,” mwanasheria alisema jana.

Kesi ya kumshurutisha Rais Kenyatta kuwateua majaji hao 41 iliwasilishwa mahakamani na wakili Adrian Kamotho Njenga.

Katika kesi hiyo Bw Njenga alikuwa ameomba mahakama itangaze hatua ya Rais Kenyatta kukataa kuwateua majaji hao ni ukandamizaji wa haki za majaji waliohitimu na pia kuathiri utenda kazi katika idara ya mahakama.

Pia wakili huyo alisema katika kesi hiyo kuchelewesha kuapishwa kwa majaji hao na Rais Kenyatta ni ukiukaji wa katiba.

Mahakama iliombwa imshurutishe rais kuwateua majaji hao kwa vile kulikuwa na uhaba wa majaji katika mahakama ya rufaa na pia mahakama kuu.

Kupitia kwa wakili mwenye tajriba ya Juu Paul Muite , JSC iliwaomba majaji hao watatu wamwamuru Rais Kenyatta atekeleze majukumu yake ya kikatiba.

“Rais Kenyatta hana budi ila kutekeleza jukumu lake la kikatiba ya kuwaapisha majaji hao 41,” majaji hao walisema wakimnukuu Bw Muite alipowasilisha ushahidi mbele yao.

Bw Muite alieleza majaji hao kwamba Rais “ hana budi ila kuwaapisha majaji ambao majina yao yalipendekezwa.”

Mnamo Julai 22 Jaji Mkuu David Maraga alimpelekea majina ya Majaji 11 waliohitimu kuhudumu katika mahakama ya rufaa, majaji 20 katika mahakama kuamua kesi za mashamba na majaji 10 kuhudumu katika kesi ya kuamua mizozo ya wafanyakazi na waajiri.

  • Tags

You can share this post!

Prof Ojienda aendelee kuchunguzwa – Mahakama

Wachina watiwa adabu kwa kushambulia Mkenya

adminleo