• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
KILIMO: Anapigiwa mfano kwa kuleta ukuzaji mzuri wa mboga

KILIMO: Anapigiwa mfano kwa kuleta ukuzaji mzuri wa mboga

NA CHARLES ONGADI

AGHALABU vijana wengi punde wamalizapo masomo yao ya Kidato cha Nne huwaza kupata kazi za ofisi ama kujitosa katika biashara ya uchukuzi maarufu kama ‘Bodaboda’.

Lakini hali ni tofauti kwa kijana Derick Ochieng’, 20, ambaye mara baada ya kumaliza masomo yake ya Kidato cha Nne katika shule ya upili ya Vispa Emmanuel High iliyoko Rabuor, Kisumu, alijitosa katika kilimo biashara.

“Napenda kilimo hata nikiwa shuleni nilipenda sana somo la kilimo ndiposa nilipokamilisha masomo niliamua kujihusisha na kilimo,” asema Ochieng’.

Bila kupoteza muda, Ochieng’ aliamua kujiunga na Magwar Ber Farm iliyoko pembezoni mwa barabara kuu ya Kisumu/Nairobi mita chache kutoka kituo cha biashara cha Rabuor kama mmoja wa wafanyikazi kwa lengo la kupalilia zaidi ujuzi wake katika kilimo.

Tangu ajiunge na Magwar Ber Farm, Ochieng’ ameweza kuleta mabadiliko makubwa akivumbua mbinu bora ya kilimo cha pilipili mboga, sukumawiki na spinachi ambazo awali hazikuwa zikifanya vizuri eneo hili.

“Wakulima wengi eneo hili walikuwa na dhana kwamba mboga za sukuma wiki, spinachi na pilipili hoho haziwezi kufanya vyema licha na kuwepo kwa soko nzuri hapa,” aeleza.

Wakulima hapa eneo la Rabuor wanategemea sana kilimo cha mahindi wanayoamini ndiyo inayofanya vyema na ni tegemeo kwa chakula.

“Nilizungumza na mkurugenzi wa shamba hili Peter Ojuka kuhusu umuhimu wa kuchimba kisima cha maji kwa minajili ya kunyunyizia maji shamba letu kipindi cha kiangazi hasa tunapoendeleza kilimo cha pilipili mboga, sukumawiki na spinachi,” aeleza.

Ochieng’ anaelezea Akilimali kwamba ili kupata pilipili mboga nzuri na ya kuvutia wateja, kwanza anapanda mbegu katika nasari inayochukua wiki tatu kuchipuka.

Baada ya pilipili mboga kuanza kumea katika nasari anazihamisha katika shamba lililotayarishwa vilivyo lililo na mbolea aina ya samadi ama fatalaiza aina ya Yara Winner ama Nitrabor iliyowekwa mwezi mmoja kabla.

Ochieng’ anaongeza kwamba pilipili mboga huchukua miezi mitatu pekee kuwa tayari kuvunwa na mkulima kupata faida yake.

Aidha, anakiri kwamba kuna changamoto ambazo mkulima ni lazima ajihadhari nazo mapema hasa wadudu wanaovamia mizizi na matawi ya pilipili mboga yanapokuwa shambani.

Mkulima asipokuwa mwangalifu kwa kukabili mara moja wadudu hao kwa dawa hitajika, basi wanaweza kuzua hasara kubwa.

Hali imekuwa hivyo hata kwa mboga za sukumawiki na spinachi ambazo wakulima wengi eneo hili hawakuamini inaweza kufanya vyema.

Anasema kwamba sukumawiki na spinachi huchukua siku tano pekee kuchipuka katika nasari kisha zikamaliza kati ya wiki tatu ama mwezi kuanza kuvunwa.

“Zamani wakazi wengi hapa walitegemea kununua sukumawiki na spinachi kutoka maeneo mengine ama kusafiri hadi Kisumu kununua bidhaa hii lakini tangu nianzishe kilimo hiki nimewarahishia kazi. Wengi wanafika hapa kununua bidhaa hii,” afichua.

Hata hivyo, Ochieng’ anakiri kwamba anauza pilipili hoho kwa wingi katika soko la Jubilee iliyoko kitovuni mwa mji wa Kisumu.

Kwa siku anaweza kuvuna kati ya kilo 300 hadi 500 katika shamba la robo ekari na kuuza kwa wafanyibiashara katika soko la Jubilee kwa Sh100 kwa kilo.

Kulingana na Ochieng’ ndoto yake kuu ni kuwa na shamba lake katika siku za usoni huku akiwashauri vijana eneo la Kisumu kujitosa katika kilimo biashara.“Maisha yanazidi kubadilika na kazi za kuajiriwa na za maofisini zinazidi kupungua,” asema.

“Kwa hivyo nawashauri vijana wenzangu kutoka Kisumu na Nyanza kwa ujumla kuzamia kilimo biashara ili kwenda na wakati,” ashauri Ochieng’.

  • Tags

You can share this post!

UFUGAJI: Ulemavu kwake si kikwazo, umempa nguvu ya kujituma

Sabuni ya Kenya Kwanza

T L