• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Kiraitu aambia watu wa Gema wasahau urais

Kiraitu aambia watu wa Gema wasahau urais

Na DAVID MUCHUI

GAVANA wa Meru Kiraitu Murungi ametaka ukanda wa Mlima Kenya usahau hatua ya kutoa rais kwa kipindi cha miaka kumi ijayo na badala yake kuwashauri viongozi waimarishe vyama vya kisiasa vilivyo na mizizi eneo hilo.

Kulingana na Bw Murungi, eneo hilo linahitaji vyama vya kisiasa vyenye nguvu vitakavyosaidia kulinda maslahi yake kwa miaka 20 ijayo.

Akizungumza Jumatatu akiwa Meru wakati wa kuzindua chama cha Devolution Empowerment Party (DEP) maarufu kama Bus, Bw Murungi alisema kwamba chama chake kitapigania kaunti zitengewe pesa zaidi.

“Mlima Kenya unafaa kusahau urais kwa miaka 10 au hata 20 ijayo. Sababu yetu ya kufufua ‘Bus’ ni kuwa tuligeuzwa watazamaji katika chama cha Jubilee. Tulichukuliwa kuwa watu wa kusoma masuala ya serikali katika magazeti. Tumerejesha ‘Bus’ kwa sababu katika Jubilee, tulipoteza nguvu za kisiasa,” alisema Bw Murungi.

Alisema kupitia ugatuzi, eneo hilo litajikinga kutoka viongozi wabinafsi wanaoweza kutwaa uongozi wa nchi.

“Tunafaa kujifunza kutoka Japan ambako asilimia 60 ya bajeti ya taifa imegatuliwa. Kama pesa hizo zinaweza kuja Meru, tunaweza kutekeleza miradi mikubwa kama serikali ya kitaifa. Kutengea kaunti pesa zaidi kutawezesha masikini,” alisema Gavana Murungi.

Alisema eneo hilo linafaa kuchunga wagombea urais ambao wanaweza kurejesha Kenya enzi za utawala wa Moi wakati uchumi ulilemazwa.

“Ni lazima tujipange ili wale wanaogombea urais waje kutunyenyekea. Tunafaa kuwa pale ambapo mapato ya taifa yanagawanywa. Katika serikali ijayo, tunafaa kuwa katika meza ya kufanya maamuzi,” alisema.

Kiongozi huyo wa chama cha DEP, alisema kuwa Mlima Kenya unakumbwa na hatari ya kukosa usemi iwapo viongozi wake watagawanyika na kufuata maslahi ya kibinafsi.

“Chini ya Jubilee, tumekosa sauti na nguvu za kisiasa. Lazima turejeshe watu wetu katika njia iliyo sawa. Tukiungana katika Bus, eneo la Mlima Kenya Mashariki litakuwa na kura 1.5 milioni za kutumia kujadiliana na wale wanaotafuta urais. Wakija, tutawapa matakwa yetu kwa maandishi,” alisema Bw Murungi.

Alieleza kwamba wanachama wa DEP watachagua mgombea urais wanayetaka mapema mwaka 2022 baada ya kushauriana kwa mapana.

Maafisa wa DEP pia walianza kusajili wanachama wapya chama kinapojiandaa kuwa na wawaniaji wenye nguvu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Bw Murungi aliongeza kwamba chama hicho kinataka kuzoa kura nyingi katika kaunti za Embu, Tharaka Nithi, Meru na Isiolo kando la kutafuta uungwaji mkono kote nchini.

You can share this post!

Mulomi atangaza azma yake kurithi kiti cha Ojaamong

Kimemia pabaya washirika wakizidi kumkosoa

T L