• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
Machafuko Sudan yasababisha changamoto kubwa za kibinadamu

Machafuko Sudan yasababisha changamoto kubwa za kibinadamu

Na MASHIRIKA

KHARTOUM, Sudan

MILIO ya risasi iliendelea kusikika Ijumaa jioni katika jiji kuu Khartoum ingawa awali, wanajeshi wa vikosi pinzani walitangaza kuwa wangesitisha mapigano kutoa nafasi kwa sherehe za Idd.

Wanajeshi waaminifu kwa naibu mkuu wa majeshi Hamda Daglo, ambaye ni kamanda wa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF), walisema walikuwa tayari kuruhusu kufunguliwa kwa viwanja vya ndege kutoa nafasi kwa usafirishaji raia wa kigeni kutoka Sudan.

Umoja wa Mataifa (UN), Amerika, Uingereza, Japan, Uswisi, Korea Kusini, Uswidi na Uhispania zimesema zinajiandaa kuondoa wafanyakazi wao nchini Sudan wasijeruhiwe katika mapigano hayo ambayo yamedumu kwa wiki moja sasa.

Zaidi ya watu 400 wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika vita hivyo kati ya wanajeshi watiifu kwa Mkuu wa Majeshi Abdel Fattah al-Burhan na wale watiifu kwa naibu wake, Jenerali Hamdan Daglo.

UN inasema machafuko Sudan yamesababisha changamoto kubwa za kibinadamu katika taifa hilo ambalo hutegemea chakula cha msaada.

Mapigano makali yaliendelea kati ya vikosi pinzani vya wanajeshi katika vitongoji vya wakazi wengi kati na kaskazini mwa Khartoum, mashahidi walisema, huku watu wengi wakisalia manyumbani bila maji, chakula na umeme.

Mapigano yaliendelea licha ya wanajeshi wa pande zote mbili kuahidi kuheshimu miito ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Amerika Antony Blinken ya kusitisha vita “angalau kwa siku tatu kutoa nafasi kwa sherehe za sikukuu ya Idd ul-Fitr.

Blinken alisema viongozi wa kijeshi na wale wa makundi ya kiraia sharti waanzishe mazungumzo ya kurejesha amani Sudan ili kuzuia kusambaratika kwa nchi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Miili mingine 14 yafukuliwa katika shamba la Mackenzie

Wakazi Murang’a waonywa kuhusu kachumbari kolera...

T L