• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
Majambazi 5 sugu wauawa Mombasa

Majambazi 5 sugu wauawa Mombasa

Na MOHAMED AHMED

MAJAMBAZI watano hatari waliokuwa wakijifanya waumini wa kanisa moja kuficha vitendo vyao, waliuawa Jumamosi eneo la Bomboululu, Mombasa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi wa kitengo maalum cha kupambana na uhalifu.

Maafisa wa kitengo hicho maalum walitoka Nairobi kupambana na majambazi hao ambao wanaaminika kuhusika katika visa vingi vya uhalifu jijini Mombasa.

Inashukiwa ni genge hilo lililowapora wafanyabiashara zaidi ya Sh1.7 milioni katika visa tofauti vilivyotokea jijini Mombasa.

Jumamosi, operesheni ya maafisa hao ilianza saa kumi na moja alfajiri hadi saa moja unusu asubuhi ambapo majambazi hao walimiminiwa risasi na kuuawa.

Kamanda wa polisi eneo bunge la Nyali,Daniel Mumasaba alisema kuwa bunduki aina ya AK47 pamoja na risasi 32 zilipatikana katika nyumba ambayo majambazi hao walikuwa wanajificha

“Hili ni genge ambalo limekuwa likisumbua wakazi na kutekeleza mashambulizi katika maeneo ya Kisauni, Nyali na Likoni. Walifikisha mashambulizi yao hadi karibu na mpaka wa Tanzania, lakini leo tumewapata baada ya kujulishwa kuwa wako eneo letu,” akasema Bw Mumasaba.

Kulingana na ripoti ya ujasusi ilionekana na Taifa Jumapili, majambazi hao walitambuliwa kwa majina ya Benedicto Kago Mugure anayefahamika kama General, Michael Kimani Njoroge anayefahamika kama One Man Army, Newton Kibara Ndege anayefahamika kama Kaparo, Bakari Hassan Mwagandi maarufu kwa jina Beka and Salim Tsuma Ndegwa anayejulikana kwa jina maarufu Kidevu.

Ripoti hiyo ilisema kuwa watano hao wamekuwa wakiendesha operesheni zao za uhalifu na kujifanya kuwa waumini wa kanisa la River Trinity Miracle Church lililoko mita chache na nyumba ambayo wamekuwa wakitumia kama maficho.

Viongozi wa kundi hilo walitajwa kuwa “Pasta” John Kamau Mugwe na naibu wake Lawrence Kathura Kamau kwa jina jingine Mzee Kibaki ambao walikuwa hawapo wakati wa operesheni ya jana.

Polisi wameanzisha msako dhidi ya wawili hao ambao wanaaminika kuingia mafichoni. Kulingana ripoti za usalama Lawrence amekuwa katika mawasiliano na maafisa wa polisi eneo la Nairobi ambao wamekuwa wakiwasaidia na risasi ambazo wanatumia katika mashambulizi yao ya uhalifu.

Miongoni mwa mashumbulizi ya genge hilo ni pamoja na yale yaliyotokea miezi tofauti mwaka jana ambapo waliibia wafanyabiashara kadha.

  • Tags

You can share this post!

Watahiniwa watasaidiwa kusafiri – Oguna

Wakurugenzi wa shirika la KTDA wakataa kutuliza boli