• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Mamilioni katika hatari ya kufa njaa Kenya, Ethiopia…

Mamilioni katika hatari ya kufa njaa Kenya, Ethiopia…

NA AFP

NEW YORK, AMERIKA

WATU milioni 20 katika nchi tatu za upembe wa Afrika, ikiwemo Kenya, wako katika hatari ya kuangamia kutokana na makali ya njaa, Umoja wa Mataifa umeonya.

Ripoti ya Shirika la Chakula Duniani (WFP) inaonyesha kuwa idadi ya watu wanaohangaishwa na njaa katika nchi za Ethiopia, Kenya na Somalia inaongezeka kila siku.

Shirika hilo linasema kuwa ukame wa muda mrefu umetatiza shughuli za kilimo na kuangamiza mifugo, hivyo kuongeza idadi ya watu wanaohitaji chakula cha msaada kwa dharura.

“Mvua isiponyesha mwezi huu, idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula itaongezeka kutoka milioni 14 sasa hadi milioni 20 mwishoni mwa mwaka huu,” ikaonya ripoti ya WFP.

Ilisema kuwa watu milioni 6 nchini Somalia wanahangaishwa na makali ya njaa na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka katika muda wa miezi minne ijayo.

Nchini Kenya, watu milioni 3.2, haswa maeneo ya Kaskazini Mashariki, wanakumbwa na njaa huku maelfu ya wafugaji wakiwa wamepoteza mifugo wao.

Hali ni mbaya zaidi nchini Ethiopia ambapo idadi kubwa ya watu wasiokuwa na chakula imesababishwa na ukame na mapigano ya miezi 17 baina ya wanajeshi wa serikali na waasi wa kundi la TPLF.

Ripoti hiyo inasema kuwa vita vya Ukraine vinavyoendeshwa na Urusi pia vimechangia katika ongezeko la baa la njaa katika mataifa ya upembe wa Afrika.

Ethiopia na Somalia hutegemea kwa kiasi kikubwa vyakula kutoka Ukraine na Urusi.

Shirika la WFP lilisema kuwa bei ya vyakula nchini Ethiopia imeongezeka kwa asilimia 66 na Somalia kwa asilimia 36 tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

WFP ilitoa ripoti hiyo huku Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) likiyataka mataifa kutarajia bei ya juu ya bidhaa muhimu kutokana na vita vya Ukraine.

IMF ilitoa onyo hilo huku wanajeshi wa Urusi jana Jumatano wakizidisha mashambulio katika bandari ya Mariupol, Ukraine ambapo zaidi ya watu 100,000 wamekwama.

IMF ambayo hukopesha zaidi ya mataifa 190 duniani imesema kuwa vita hivyo vya Ukraine vinavyoendelezwa na Urusi vitapunguza kasi ya ukuaji wa uchumi duniani kutoka asilimia 6.1 hadi asilimia 3.6 mwaka huu.

Shirika la IMF katika ripoti yake lilisema kuwa vita nchini Ukraine vitafanya bei ya bidhaa muhimu kama vile mahindi, ngano, gesi, mafuta ya kupikia na vyuma kupanda zaidi.

Urusi pamoja na Ukraine huzalisha kiasi kikubwa cha bidhaa hizo muhimu.

Jana Jumatano, mapigano yalichacha katika bandari ya Mariupol baada ya wanajeshi wa Ukraine katika mji huo kukataa kujisalimisha kufikia jana Jumatano saa sita mchana kama walivyotakiwa na Urusi.

Kamanda wa majeshi ya majini Serhiy Volyna alisema kuwa wanajeshi zaidi ya 500 waliozingirwa na majeshi ya Urusi mjini Mariupol hawatajisalimisha huku akiomba jamii ya kimataifa kuwaokoa.

  • Tags

You can share this post!

VALENTINE OBARA: Piga kura uchaguzini, usipige domo kuhusu...

Joho aaga wakazi wa Mombasa

T L