• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 3:55 PM
Manduku akamatwa

Manduku akamatwa

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) Daniel Manduku amekamatwa Alhamisi jioni kufuatia amri ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji.

Manduku amekamatwa kuhusiana na sakata ya utoaji zabuni ya thamani ya Sh224 milioni katika mamlaka hiyo bila kufuata sheria na sera zinazohitajika.

Anazuiliwa katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Nairobi akisubiri kuwasilishwa mahakamani kujibu mashtaka ya ufisadi.

Atashtakiwa pamoja na Juma Fadhili Chugulu – afisa wa ujenzi katika KPA – ambaye aliidhinisha malipo kutokana na ununuzi wa bidhaa kinyume cha sheria.

Kwenye taarifa aliyoitoa Alhamisi asubuhi, Bw Haji alisema uchunguzi umebaini kuwa Bw Manduku aliidhinisha utengenezaji wa “concrete barriers” za kujenga ua katika depo ya kuweka makontena (ICD), Bandari ya Kilindini na sehemu ya kuweka bidhaa iliyoko Makongeni ilhali mpango haukuwa kwenye bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2018/2019.

Vile vile, DPP anasema zabuni hizo za utengenezaji mawe ya kujenga ua zilipewa kampuni 10 ambazo ziliteuliwa na Bw Manduku kinyume na sheria za ununuzi wa bidhaa na huduma za umma.

Wapelelezi waligundua kuwa KPA ilitoa malipo yaliyopita kiwango kinachohitajika kwa Sh244.8 milioni kwa wakandarasi hao kwa kazi ambayo haikukamilishwa.

“Kwa hivyo, nimeridhika kuwa kuna ushahidi wa kutosha wa kuwezesha mashtaka dhidi ya Daniel Manduku aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa KPA na Juma Fadhili Chigulu aliyekuwa Afisa wa Ujenzi, KPA,” akasema Bw Haji.

You can share this post!

Sabina Chege apinga mpango wa elimu mashinani

Jumwa kukamatwa kwa tuhuma za ufisadi