• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
MLO MTAMU: Wali, kuku na mkate aina ya naan

MLO MTAMU: Wali, kuku na mkate aina ya naan

NA MARGARET MAINA

[email protected]

IKIWA unatafuta njia ya kubadilisha utaratibu wako wa kuandaa chakula basi shughuli nzima ya kupika wali, kuku na mkate aina ya naan itakupa tabasamu usoni.

Muda wa kuandaa: Dakika 2o

Muda wa mapishi: Dakika 40

Walaji: 4

Vinavyohitajika

  • vijiko 2 vya mafuta
  • kitunguu maji 1 kilichokatwa
  • kijiko 1 cha tangawizi safi iliyokatwa vizuri au iliyokunwa
  • kitunguu saumu punje 10 iliyosagwa
  • nyama ya kuku yenye uzani wa pauni 1 ½ na isiyo na mfupa na iliyokatwa vipande vipande
  • nyanya 7 au mchuzi wa nyanya
  • kijiko 1 cha garam masala
  • kijiko 1 cha paprika
  • kijiko 1 cha fenugriki ya unga (hiari)
  • kijiko ½ cha cumin
  • chumvi
  • kijiko ¼ pilipili nyeusi
  • kikombe ½ cha krimu nzito na ½ mtindi
  • kikombe 1 ½ mchele wa Basmati au Jasmine
  • maji kiasi
  • kinyunya cha unga wa ngano
  • kikombe cha majani ya giligilani na ambayo yamekatwakatwa
  • vijiko 3 vya siagi iliyoyeyuka

Maelekezo

Kupika kuku kwa siagi

Pasha moto wa wastani kisha injika sufuria. Mimina mafuta kwenye sufuria halafu utumbukize ndani vitunguu. Kaanga vitunguu hadi viwe na rangi ya dhahabu; itakuchukua muda wa kama dakika nne. Ongeza tangawizi na kitunguu saumu kiasi na upike kwa sekunde 30 huku ukikoroga ili visiungue. Ongeza kuku, nyanya, na viungo. Pika kwa muda wa dakika sita au mpaka kila kitu kiive. Ongeza krimu nzito na chemsha kwa dakika 10 huku ukikoroga mara kwa mara.

Kupika naan

Mkate aina ya naan. PICHA | MARGARET MAINA

Changanya vitunguu, siagi, na giligilani kwenye bakuli ndogo. Weka kando. Gawanya kinyunya cha unga sehemu nane sawa. Pinda unga uchukue umbo la mduara mdogo kwa kutumia mpini wa kusukumia. Pasha kikaangio kwa moto wa juu na upake mafuta kidogo kwenye kikaangio ili unga usishikamane na sufuria. Weka naan kwenye kikaangio na pindua kisha ueneze mchanganyiko wa siagi, majani ya giligilani na vitunguu. Pika hadi mkate aina ya naan uive kisha rudia mpaka unga wote uishe.

Wali

Osha mchele kisha suuza. Katika sufuria, yaache maji yachemke kisha ongeza mchele. Punguza moto, funika na upike kwa muda wa robo saa. Zima moto na wali utulie kwa dakika tano.

Pakua mlo wako na ufurahie.

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Supu ya broccoli na jibini ya Cheddar

MAPISHI KIKWETU: Tacos zenye nyama ya kuku iliyookwa

T L