• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Msichana, 12, ndani kwa dai la kumuua mpenziwe

Msichana, 12, ndani kwa dai la kumuua mpenziwe

Na BENSON MATHEKA

MSICHANA wa miaka 12 anayeshukiwa kumuua mpenzi wake mwenye umri wa miaka 19 mtaani Langata, Nairobi, atazuiliwa seli za polisi kwa siku tano zaidi.

Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Kibera, Bi Esther Boke, aliwapa polisi muda huo walipowasilisha ombi waendelee kumzuilia mshukiwa ili wampeleke akapimwe hali ya akili.

Kwenye ombi lao, polisi walisema msichana huyo aliokolewa na afisa wa mpango wa Nyumba Kumi wakazi walipomvamia wakitaka kumuua.

Mahakama iliagiza polisi wahakikishe usalama wake akiwa seli kwa kumtenga na washukiwa wengine ambao ni watu wazima.

Msichaha huyo alikamatwa Jumatano kwa kushukiwa kumuua mvulana huyo kwa kumdunga kisu kifuani.

Kulingana na polisi, kisa hicho kilitendeka baada ya msichana huyo mwanafunzi wa darasa la sita kugombana na mvulana huyo.

Majirani walifahamisha polisi kwamba wawili hao walitofautiana kabla ya msichana huyo kumdunga kisu mvulana huyo mara mbili kifuani.

Majirani walisema kwamba walisikia kamsa kutoka ndani ya nyumba ambayo wawili hao walikuwa, na walipoenda kuangalia, walimpata mvulana huyo akivuja damu kwa wingi.

Walifahamisha polisi kwamba mwathiriwa na msichana huyo walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.

Walisema kwamba msichana alikuwa akimtembelea mvulana huyo mara kwa mara mchana.

Haikufahamika mara moja kilichozua ugomvi kati yao ingawa baadhi ya majirani waliambia polisi kwamba msichana alikuwa amemlaumu mvulana kwa kuwa na uhusiano na msichana mwingine.

Mkuu wa polisi eneo la Langata, Gregory Mutiso alisema msichana huyo alikamatwa kuhusiana na mauaji ya mvulana huyo.

Mvulana huyo alikufa akipelekwa hospitali ya St Mary’s mtaani Otiende.

Madaktari katika hospitali hiyo walisema alikuwa ametokwa na damu kwa wingi.

Msichana huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Langata na atafikishwa kortini uchunguzi ukikamilika. Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika mochari ya City.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge wakataa mswada unaolenga kuwapa madiwani nafasi...

Afa lojing’i akiwa na jamaa