• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Msitu wa Arsenal kunyanyua hadhi ya kijiji cha Shingwaya

Msitu wa Arsenal kunyanyua hadhi ya kijiji cha Shingwaya

NA MAUREEN ONGALA

KWA miaka mingi, kijiji cha Shingwaya kilichoko eneo la Bore, eneobunge la Magarini, Kaunti ya Kilifi, kilikuwa miongoni mwa vijiji ambavyo vimetengwa sana kimaendeleo.

Matatizo chungu nzima kama vile njaa tele wakati wa kiangazi kinachodumu kwa muda mrefu na mafuriko wakati mvua inapokunya, yalikuwa kama ibada sawa na ilivyo katika maeneo mengi ya Kilifi.

Umaskini wa kupindukia ulisababisha wakazi kukata miti ovyo ili wachome makaa ndipo wajipatie riziki, lakini matokeo yake yalikuwa uharibifu zaidi wa mazingira na hivyo kusababisha mahangaiko zaidi wakati wa kiangazi na mafuriko.

Hata hivyo, eneo zima la Bore sasa limeanza kupata mandhari mapya baada ya klabu ya kandanda ya Uingereza ya Arsenal kupiga jeki mradi wa upandaji miti katika juhudi za kukabili athari za tabianchi inayozidi kuathiri ulimwengu.

Hatua hii ya Arsenal inaendelezwa huku zaidi ya kaunti 12 ikiwemo Kilifi zikiendelea kukumbwa na janga la ukame mkali uliosababishwa na ukosefu wa mvua tangu mwaka uliopita.

Katika Kaunti ya Kilifi, vidimbwi vya maji vimekauka huku wakazi wakilazimika kutembea kwa mwendo mrefu kutafuta maji ya kutumia pamoja na mifugo yao.Wakazi hao pia wamekosa chakula baada ya mimea waliyopanda kunyauka na kukosa kunawiri kutokana na ukosefu wa mvua.

Mradi huu wa upandaji miti unatajariwa kuzalisha msitu utakaoitwa ‘The Arsenal Forest in Africa’ na unaendeshwa kwa ushirikiano na shirika lisilo la serikali la Carbon Link linalojihusisha na masuala ya kutunza na kuhifadhi misitu na lile la Bore Green Umbrella kwa niaba ya klabu hiyo, miongoni mwa mashirika mengine likiwemo Shirika la Kuhifadhi Misitu nchini Kenya (KFS).

Shirika la Carbon Link husaidia jamii mbalimbali nchini kuendeleza upanzi wa miti.Akizungumza na wanahabari, Bw Ru Heartfelt kutoka nchi ya Wales ambaye anahusika katika mradi huo alisema Arsenal inalenga kuwaonyesha mashabiki wao walio Uingreza kuwa wanawasaidia mashibiki wao barani Afrika ambao ni wengi.

“Hili ni tendo la hisani kutoka kwa klabu ya Arsenal ambayo inawatambua mashabiki wake walio katika bara la Afrika,” akasema.Bw Heartfelt alisema kwamba kwa muda sasa amekuwa akitafuta msaada wa fedha kutoka ng’ambo ili kusaidia jamii kuendeleza miradi ya maendeleo kuwafaidi watu maishani.

Alisema kuwa kwa miaka mingi tokea miaka ya tisini, alikuwa anapanda miti kwa minajili ya kufyonza gesi ya carbon kabla ya kuja nchini Kenya.

Hii ni baada ya utafiti uliofanywa nchini Amerika kubaini kwamba misitu aina ya tropiki inayopatikana barani Afrika inachangia pakubwa katika kuimarisha mazingira.

“Niliacha kupanda miti kwetu Uingereza na kuja nchini Kenya kuanzisha upanzi wa miti ya misitu ya tropiki,” akasema Bw Heartfelt.

Alisema kuwa Arsenal inagharimia upanzi wa miti katika shamba ekari 12.5 ambayo ni takriban asilimia 21.3 ya viwanja vya Emirates kule London.

Aliongeza kuwa wamekuwa wakifanya kazi na kikundi cha jamii cha Bore kwa zaidi ya miaka 14 katika juhudi za kuimarisha msitu ulioharibiwa na pia kupanda miti katika maeneo mbalimbali vijijini katika sehemu ya Shingwaya.

Hatua hii ni katika juhudi za kuongeza idadi ya miti katika eneo hilo. Alisema kwamba katika miaka hiyo, wamefanikiwa kuongeza upanzi wa mikanju na wanaendelea kusaidia takribani wakazi 400 katika njia mbalimbali kujikimu maishani.

“Miti hii itasaidia kufyonza kiwango kikubwa cha hewa ya carbon kwa miaka 25 ijayo na pia itarejesha zile karatasi tulizotumia kuchapicha ratiba za mechi ya Arsenal,” akasema.

Pia, wamewapa takriban wakulima 3,000 miche na wanalenga kufikia shule 460 katika Kaunti ya Kilifi.Kwa mujibu wa Bw Heartfelt, wanapanda miti ambayo inastahimili ukame kama vile mwarubaine. Alisema mojawapo ya jukumu lake ni kuwashawishi raia wa nchi zilizojiendeleza kutambua umuhimu wa kusaidia na kuwezesha jamii maskini kuhifadhi misitu.

Bw Heartfelt alisema ufadhili kutoka klabu ya Arsenal ulikuja kwa bahati tu baada ya mwanachama mmoja wa kujitolea katika shirika la Carbon Link kujitwika jukumu la kutoa madaftari ya mechi za timu hiyo huko Uingereza kwa jamii.

Kupitia hatua hiyo, timu ya Arsenal iliwasiliana na shirika hilo na kuliuliza iwapo lilikuwa radhi kupanda miti kama njia moja ya kulipia raslimali walizotumia.

“Tulikubali ombi hilo na tumeanza kupanda miche 20,000 na mradi huu utatoa ajira kwa wanajamii kwa kupanda miti, kufyeka misitu na kunyunyizia maji miche hiyo,” akasema Mbali na kufadhili mradi wa upanzi wa miti, klabu hiyo iliwatunuku wachezaji wa timu ya mpira ya Bore Shingwaya mipira, viatu vya kuchezea na jezi ili kupga jeki vipaji.

Bw Alex Katana kutoka kikundi cha jamii cha Bore alisema lengo kuu halikuwa kupanda miti tu, bali kutoa nafasi za ajira kwa wanajamii ili kuwawezesha kupata pato la kila siku.

Walianzisha mipango ya kujenga madarasa katika shule za eneobunge hilo na pia kuwezesha jamii kuweka umeme wa kutumia miale ya jua.

Mbali na hayo, kikundi hicho kimeanzisha hoteli ya watalii katika eneo la Bore kama kitega uchumi kwa kutoa nafasi za kazi ili kupunguza uharibifu wa misitu kwa kuchoma makaa.

Alisema kwamba kwa miaka mitano ijayo, wanalenga kurejesha miti yote iliyokatwa kwa kutumia mbinu ya kipekee ya kufanya makubaliano na jamii kuwa watapata pesa na hawatakata miti kwa minajili ya kuchoma makaa

.Bw Lenox Katana wa kijiji cha Bore Singwaya alielezea furaha yake kuwa eneo hilo limepata hadhi tena ikilinganishwa na wakati ambapo miti ilikatwa na kuacha ardhi kavu.

“Wakazi wengi wameelimishwa kuhusu umuhimu wa misitu na kuwezeshwa kupata njia mbadala ya kupata pesa ili wasikate miti,” akasema.

Kwa upande wake, Bw Idriss Maalim, ambaye ni msaidizi wa mbunge wa Magarini, Bw Michael Kingi, alipongeza klabu ya Arsenal na kusema kuwa mbali na kulinda mazingira, mpango huo utasaidia katika kukuza vipaji vya soka katika eneobunge hilo.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wa ODM wakana kulegea

Mikakati yake Uhuru kuzima Ruto Mllimani

T L