• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:10 PM
Nauli ghali tena Wakenya wakiendelea kupambana na maisha

Nauli ghali tena Wakenya wakiendelea kupambana na maisha

NA WANDERI KAMAU

WAKENYA wanaosafiri kwa magari ya matatu kuanzia leo Jumatano wanahisi makali ya Sheria mpya ya Fedha 2023, baada ya Chama cha Wenye Matatu Kenya (MOA) kutangaza kuongeza nauli kote nchini.

Chama hicho kilitangaza Jumanne kuwa, hatua hiyo imechangiwa na athari za kupitishwa kwa mswada huo, ambapo moja ya matokeo hayo ni kupandishwa kwa bei ya mafuta.

Ijumaa wiki iliyopita, Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Mafuta (EPRA) iliongeza bei za petroli, dizeli na mafuta taa kwa Sh13.49, Sh12.39 na Sh11.96 mtawalia.

EPRA ilifanya hivyo licha ya Mahakama Kuu ya Nairobi kusimamisha utekelezaji wa Sheria hiyo hadi kesi isikizwe na kuamuliwa.

Kwa sasa, bei ya lita moja ya petroli, dizeli na mafuta taa ni Sh195.53, Sh179.67 na Sh173.44 mtawalia jijini Nairobi na maeneo mengine nchini.

Kutokana na hatua hiyo, Wakenya wanaokaa na kufanya kazi jijini Nairobi au viungani mwake watalazimika kuongeza nauli wanayolipa kwa sasa kwa kati ya Sh10 na Sh30.

Kwa wale wanaosafiri kutoka jijini hadi katika kaunti jirani kama Kajiado, Machakos, Murang’a na Kiambu, nauli zao zitaongezwa kwa kati ya Sh20 na Sh50.

Katika eneo la Pwani, wananchi wanaosafiri kutoka jijini Mombasa hadi katika maeneo kama Voi, Malindi, Ukunda, Kilifi, Lamu, Tana River, Wundanyi na Mwatate, nauli zitaongezwa kwa kati ya Sh30 na Sh70.

Katika eneo la Nyanza, linalojumuisha njia za kutoka; Nairobi-Kisumu, Kisumu-Nairobi, Nairobi-Homa Bay, Migori-Nairobi na Nairobi-Kisii, nauli zitaongezwa kwa kati ya Sh100 na Sh200.

Katika eneo la Bonde la Ufa, wale wanaosafiri jijini Nairobi kuelekea katika maeneo kama Kitale, Bomet, Kericho, Narok, Kapenguria, Baringo, Eldoret, Nakuru, Kapsabet na Naivasha, nauli zao zitaongezwa kwa kati ya Sh100 na Sh200.

Kwa wale wanaosafiri kutoka jijini Nairobi hadi katika maeneo ya Kati (Mlima Kenya Magharibi) kama Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Nyandarua, Laikipia na Nyahururu, nauli zao zitaongezwa kwa Sh150.

Wale wanaosafiri kutoka Nairobi hadi maeneo ya Meru, Embu na Isiolo (Mlima Kenya Mashariki), wataongezwa nauli zao kwa kati ya Sh100 na Sh150. Mwishowe, wale wanaosafiri kutoka Nairobi hadi maeneo ya Magharibi kama Kakamega, Bungoma, Busia, Vihiga na Mumias, nauli zao zitaongezwa kwa kati ya Sh200 na Sh300.

Kwenye kikao na wanahabari, mwenyekiti wa chama hicho, Bw Albert Karakacha, alisema walilazimika kufanya hivyo, ingawa wanafahamu hali ngumu ya maisha wanaopitia Wakenya.

“Tunajua hali ya kiuchumi ni ngumu kwa kila Mkenya. Hata hivyo, hatuna uamuzi mwingine kwani hata sisi tumelazimika kununua mafuta ya magari kwa bei ya juu,” akasema Bw Karakacha.

Hali hiyo inajiri huku ripoti iliyotolewa jana na shirika la utafiti la Trends and Insight for Africa (TIFA) ikionyesha kuwa, Wakenya wengi wameanza kutumia kuni badala ya mafuta kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha.

“Ingawa idadi kubwa ya Wakenya bado wanatumia kuni kwa matumizi muhimu kama kupikia (asilimia 45), wengi wamelazimika kufanya hivyo kutokana na gharama ya juu ya mafuta,” akasema jana Jumanne Mtafiti Mkuu wa shirika hilo Dkt Tom Wolf.

  • Tags

You can share this post!

Wito makundi ya CSOs yaungane na Azimio kwa mkutano wa Saba...

Ingwe ya msimu ujao ni wembe – Shikanda

T L