• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Ngamia, mnyama ambaye manufaa yake hayakadiriki

Ngamia, mnyama ambaye manufaa yake hayakadiriki

Na KENYA NEWS AGENCY

JAMII ya waSomali ambayo inaishi Kaskazini Mashariki ya Kenya ni kati ya zile jamii ambazo zinashiriki ufugaji wa kuhamahama katika eneo hilo kame.

Kutokana na mtindo huo wa maisha, jamii hii imejizolea umaarufu kutokana na ufugaji wa ngamia, mnyama ambaye anaweza kustahimili kuishi na kutembea katika mazingira haya kame.Mbali na ngamia, jamii hii pia hushiriki ufugaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo ambao pia wao huhama nao kutoka eneo moja hadi jingine wakitafuta malisho hasa nyakati ambapo kiangazi kimekithiri zaidi.

Ni mtindo wa maisha ambao pia umezoeleka sana katika kaunti za Garissa, Mandera, Wajir, Turkana sehemu za Tana River, Samburu na Narok na sehemu za Kaunti ya Kajiado. Kando na Wasomali, Waborana, Wamaasai, Wasamburu, Waturkana pia hushiriki katika ufugaji huo wa kuhamahama ambao umekuwepo tangu jadi.

Hata hivyo, ni ufugaji wa ngamia ambao umesaidia sana katika kukimu maisha ya Wasomali kutokana na manufaa mengi yanayoandamana na ufugaji wa mnyama huyo.Wasomali huwakama ngamia kupata maziwa, huwachinja kwa ajili ya nyama yao inayosemekana ni laini na tamu, huwatumia wakati wa kusafirisha mizigo kutoka eneo moja hadi jingine na hata ngozi ya mnyama huyu hutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali miongoni mwa jamii ya Wafugaji ambazo baadaye huuzwa madukani.

Miongoni mwa jamii ya Wasomali, mkulima au familia hustahiwa sana kutokana na idadi ya ngamia ambao wamewafuga. Iwapo familia imewafuga ngamia wengi, hiyo huchukuliwa kama ishara kuwa wana mali nyingi na familia husika hutunukiwa heshima huku wanaume wakipewa uongozi katika mabaraza ya wazee yanayotoa uamuzi kuhusu masuala mbalimbali katika jamii.

Zaidi ya hayo, jamii huandaa sherehe za kitamaduni ambako nyimbo za kuwasifia ng’amia hao huimbwa. Wanaume wanaoenda kuoa vilevile huheshimiwa sana wakitoa ngamia kama mahari na wao huthaminiwa sana na familia ya msichana hasa mwanamume akitoa idadi yao kubwa ngamia badala ya mifugo wengine.I

sitoshe, mizozo mingi kati ya wanajamii husuluhishwa na wazee na aliyemkosea mwenzake mara nyingi huomba radhi kisha hutozwa faini ya ngamia. Vilevile, kuna tamaduni ambayo huhusisha mashindano ya ngamia ambayo bado huandaliwa kila mwaka na Wasomali.

Aidha, ngamia hutunzwa sana na jamii ya Wasomali kutokana na amri ya tamaduni yao na umuhimu wake wakati wa sherehe za kidini na pia za mashindano ya urembo. Kwa mujibu wa Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo (KALRO), Kenya ina ngamia 3,338, 757 na inashikilia nafasi ya nne ulimwenguni baada ya Chad, Somalia na Sudan.

Idadi ya Ngamia

Hapa nchini, Mandera inaongoza kwa idadi ya ngamia 1, 016, 970 ikifuatwa na Turkana (832, 462) kisha Wajir 533,651. Vilevile, Kenya ndiyo inashikilia nafasi ya pili baada ya Somalia kutokana na kiwango cha maziwa ya ngamia. Kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) mnamo 2017, Kenya ilizalisha tani 876,224 za maziwa.

Waziri wa Kilimo na Ufugaji katika Kaunti ya Wajir, Yusuf Gedi anasema ufugaji wa ngamia umesaidia sana katika kuzuia utapia mlo kwa wakazi wa maeneo kame kwa kuwa ina virutubishi na madini ambayo husaidia kuongeza kinga mwilini.

“Maziwa ya ngamia yana kolesterol kidogo, aina mbalimbali ya madini na aina ya vitamini C. Ni maziwa yenye manufaa sana mwilini ikilinganishwa na ya mifugo wengine. Kwa hivyo, ufugaji wa ngamia ambao ulianza na tamaduni za enzi zile, umesaidia sana jamii ya Wasomali ambao hutegemea mnyama huyo kwa mahitaji yao mengi,” akasema Bw Gedi.

Maziwa hayo pia hayaharibiki haraka kama ya ng’ombe na yanaweza kuhifadhiwa kwa siku kadhaa kwa kuwa kiwango cha asidi ndani yake pia kiko chini mno.Aidha, mtaalamu wa masuala ya kilimo na ufugaji Dkt Antony Ngugi, anaunga kauli ya Bw Gedi huku akisisitiza pia kwamba nyama ya ngamia inasaidia sana katika kutoa tiba kwa maradhi mbalimbali mwilini na pia kupunguza maumivi.

Na kwa wanaume ambao huenda wanashindwa kujimudi vyema wakati wa tendo la ndoa na wapenzi wao, nyama ya ngamia huwasaidia kwa kuwa huwaongezea nguvu za kushiriki mahaba.

Maziwa

“Maziwa ya ngamia ni bora zaidi kuliko yale ya ng’ombe kwa kuwa yana manufaa tele. Yana virutubishi na japo ladha yake huwa tofauti, yana kiwango cha wastani cha mafuta ambayo si hatari kwa mwili,” akasema Dkt Ngugi.Afisa na mtaalamu wa masuala ya ufugaji Julius Mwangi naye alifichua kuwa nyama ya ngamia huwa bora kwa sababu ina viwango vya chini vya kolestrol na mafuta mengine ikilinganishwa na ng’ombe, mbuzi au kondoo.

“Ili kupunguza magonjwa yanayoandamana na ulaji wa nyama mara kwa mara, ni vyema mtu kula nyama ya ngamia kwa kuwa inasaidia sana katika kupambana na maradhi kama shinikizo la damu na mengine ya kupumua ambayo husababisha vifo kila wakati,” akasema Bw Mwangi.

Hata kuna tofauti katika madini au virutubishi ndani ya nyama ya ngamia kulingana na umri, aina na jinsia ya ngamia ambaye amechinjwa japo kwa wastani, nyama hiyo ina proteni ambayo ina manufaa zaidi katika kusaidia mwili kuwa na kinga.

Ingawa tafiti nyingi za kisayansi zimehusisha nyama ya ngamia na tiba ya magonjwa mengi yanayotokana na mwili kuwa na mafuta mengi. Tafiti hizo zinapendekeza ulaji wa nyama hiyo japo kwa kipimo ili kusaidia kupambana na maradhi hayo.

You can share this post!

Lusaka asifu uongozi wa wanawake

Serikali yatenga Sh450m kukabili ukame

T L