• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Nyachae asifiwa kwa ushujaa wake kisiasa

Nyachae asifiwa kwa ushujaa wake kisiasa

Na WANDERI KAMAU

WAZIRI wa zamani Simeon Nyachae, Alhamisi alisifiwa kama mwanasiasa shupavu, ambaye daima alijitolea kuwapa mwongozo wenzake katika kila nyanja maishani.

Kwenye misa ya wafu iliyoandaliwa Alhamisi katika Kanisa la Maxwell SDA, Nairobi, kusherehekea maisha yake, viongozi mbalimbali waliohutubu walimkumbuka kama kiongozi mwadilifu, aliyetia bidii kazini na aliyekuwa tayari kuwapa ushauri vijana kila walipomhitaji.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni kinara wa ODM, Raila Odinga, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Martha Karua (Narc-Kenya), mawaziri Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani), Mutahi Kagwe (Afya), mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Martin Wambora kati ya wengine.

Mabwana Mudavadi, Kalonzo na Kagwe walikumbuka jinsi Mzee Nyachae alikuwa akiwapa ushauri kuhusu masuala tofauti maishani, kwani walikuwa bado vijana walipohudumu kama mawaziri kwenye serikali za marehemu Daniel Moi na Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

“Sifa moja aliyokuwa nayo (Nyachae) ni mapenzi yake kwa vijana. Baada ya vikao vya baraza la mawaziri, alikuwa akituita na kutupa miongozo kila mara alipohisi ama kuona tumekosea mahali fulani. Alikuwa kama ‘baba’ kwetu,” akasema Bw Mudavadi.

Bw Musyoka alisema ni kutokana na busara nyingi alizokuwa nazo Mzee Nyachae ambapo Bw Moi hakusita kutafuta ushauri kutoka kwake, licha ya kuwa rais.

“Mzee Nyachae alikuwa kama kito cha thamani kwa kila mmoja. Alikuwa akitoa mwongozo hata kwa Rais Moi, wakati alijipata kwenye njiapanda kuhusu masuala muhimu yaliyoihusu nchi,” akasema Bw Musyoka.

Kwa upande wake, Bw Odinga alimtaja kama kiongozi aliyetoa michango mikubwa kwenye sekta muhimu kama elimu, kilimo, biashara na utumishi wa umma.

Kwenye hotuba iliyosomwa na Bw Kagwe, Rais Uhuru Kenyatta alimtaja Nyachae kama “kiongozi wa kipekee ambaye mchango wake utakumbukwa na vizazi vijavyo.”

“Tumempoteza kiongozi aliyejituma kwa kila alilolifanya. Tunashukuru kwa maisha yake yaliyotufaa sana kama nchi,” akasema Rais.

Kauli kama hiyo ilitolewa na Dkt Matiang’i, aliyemtaja Mzee Nyachae kuwa nguzo kuu katika safari yake kwenye utumishi wa umma, hasa tangu alipoanza kuhudumu kama waziri mnamo 2013.

“Tangu nilipoteuliwa kuwa waziri, imekuwa kawaida yangu kuwasiliana na kushauriana na Mzee (Nyachae) kila mara nilipozuru nyumbani. Hakusita kutukosoa tulipokosea kama mawaziri. Ni mwaka uliopita pekee ambapo sikupata nafasi hiyo kwani alikuwa amezidiwa sana, na ilikuwa vigumu kwake kuzungumza. Amekuwa msingi muhimu wa maisha yangu katika kila hatua,” akasema Dkt Matiang’i.

Sifa kama hizo zilitolewa na wake zake, watoto na wajukuu.

Mzee Nyachae alifariki Jumatatu iliyopita, baada ya kuugua kwa muda akiwa na umri wa miaka 88.

Alihudumu katika serikali za marais Mzee Jomo Kenyatta, Moi na Kibaki kabla ya kustaafu kwenye siasa mnamo 2007.

Kwenye safari yake katika utumishi wa umma, alihudumu kama afisa wa utawala, mbunge, mkuu wa utumishi wa umma na waziri.

Atazikwa nyumbani kwake Jumatatu ijayo nyumbani kwake katika Kaunti ya Kisii.

You can share this post!

Muthama, Kalonzo wakashifiwa kwa kujibizana haflani

Majaji waogopa kazi ya Maraga