• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Pundamilia aliyetorokea kijijini sasa azaa mtoto nusu-punda, nusu-pundamilia

Pundamilia aliyetorokea kijijini sasa azaa mtoto nusu-punda, nusu-pundamilia

Na KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa kijiji cha Moa, tarafa ya Witu, Kaunti ya Lamu wamejionea pundamilia aliyetoroka msituni na kuishi pamoja na punda na ng’ombe kijijini humo akiwa amezaa mtoto ambaye ni nusu-punda, nusu-pundamilia.

Pundamilia huyo anadaiwa kutoroka kutoka msitu wa Boni hadi kijijini Moa karibu mwaka mmoja uliopita na amekuwa akiishi na mifugo na kutangamana nayo vyema kijijini humo.

Kwa mujibu wa chifu wa eneo hilo, Abdi Bocha, ambaye pia ni mfugaji aliyekuwa akimtunza mnyama huyo wa mwituni, wanakijiji hawangeweza kumfurusha pundamilia huyo kutokana na tabia zake nzuri alizokuwa akionyesha kwa mifugo wao.

Bw Bocha anasema mtangamano wake na punda huenda ndio ulisababisha yeye kujifungua mtoto ambaye ni nusu-punda, nusu-pundamilia.

“Huyu pundamilia amekuwa hapa kwangu kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi miwili sasa. Alikuwa akiishi na punda, ng’ombe, mbuzi na kondoo. Hatukumfurusha kwani tuliona amekubali na kuingiliana vyema na mazingira ya nyumbani. Jana ndipo alipojifungua mtoto ambaye upande mmoja wa mwili wake ni punda wa kawaida ilhali miguu yake ikiwa na michoro-michoro ya pundamilia. Kila mmoja amefurahishwa na kiumbe kilichozaliwa. Kinapendeza,” akasema Bw Bocha.

Barjo Dokota ambaye ni mfugaji eneo la Moa na ambaye pia amekuwa akijitolea kumtunza pundamilia huyo hadi kujifungua kwake alisema tayari wamewajulisha maafisa wa Shirika la Huduma za Wanyamapori (KWS) eneo hilo kuhusiana na tukio hilo.

“Maafisa wa kutunza wanyama wametuahidi kwamba watakuwa wakimtembelea na kumtunza pundamilia huyu na mtoto wake,” akasema Bw Dokota.

Pundamilia aliyezaa mtoto nusu-punda, nusu-pundamilia eneo la Moa, Kaunti ya Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Kwa upande wake, Kamanda wa KWS, Kaunti ya Lamu, Mathias Mwavita, alithibitisha kuzaliwa kwa mtoto huyo wa pundamilia ambaye ni nusu-punda, nusu-pundamilia.

Bw Mwavita alisema huenda pundamilia huyo alihamia katika maskani ya binadamu kukwepa kuliwa na simba msituni.

Aliwahimiza wakazi kuwakaribisha wanyama wa mwitu ambao si hatari na wanaozurura vijijini, akisisitiza kuwa Lamu imekuwa na changamoto ya maeneo finyu yanayokaliwa na wanyamapori.

“Misitu mingi imeharibiwa eneo hili na wanyama wamekuwa wakipata changamoto kwa kukosa makao. Ningewasihi wananchi kuwakaribisha wanyama pori, hasa pundamilia mijini mwao. Nafurahi kwamba pundamilia ametunzwa vyema kijijini Moa na kwa sasa ametuzalia mtoto wa kuvutia ambaye nusu-punda, nusu-pundamilia. Ni jambo zuri,” akasema Bw Mwavita.

  • Tags

You can share this post!

Jonkopings Sodra anayochezea nyota Eric Johana yazimwa...

Ibada iliyoangusha kampuni za kamari za Betin, SportPesa